Wednesday, 14 March 2018

Samia amkaribisha balozi mpya wa UfaransaMAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier ambaye aliongozana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Emmanuel Baudran.

 Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake Dar es Salaam, Balozi Clavier amewasilisha salamu za Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kwa mwenzake Dk. John Magufuli ambapo amesema ana uhakika na Tanzania ijayo na anaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli.
Balozi huyo mpya wa Ufaransa nchini amesema Rais Macron anaipongeza Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala mbali mbali ya kimataifa.
Wakati wa mazungumzo yao amemjulisha Makamu wa Rais kwamba Ufaransa inakusudia kuimarisha uhusiano zaidi na Tanzania hususan Nyanja za uchumi na siasa na kuanzisha majadiliano mbalimbali katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Balozi Clavier amemjulisha Makamu wa Rais kuwa mwezi ujao kutakuwa na ugeni ambao ni wafanyabiashara kati ya 30 au 40 kutoka Ufaransa ambao watakuja kujionea fursa mbali mbali za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini.
Balozi amemweleza Makamu wa Rais azma ya Ufaransa ya kushirikiana na vyuo vikuu vya Tanzania katika kuanzisha na kuendesha kozi mbali mbali kwa manufaa ya pande hizo mbili.
Aidha, Emmanuel Baudran amesema shirika lao linakusudia kuanzisha kiwanda cha vifaa vya umeme jua (solar) mkoani Shinyanga pia limeshafanya miradi ya uboreshaji maji taka katika manispaa ya Temeke na wanaendelea na mikakati ya uanzishwaji miradi mingine ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment