Tuesday, 13 March 2018

Serikali kuwatumbua maofisa habari wazembe


Dk. Harrison Mwakyembe

Mwandishi Wetu,Arusha

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema atawasilisha kwa Waziri Mkuu majina ya maofisa habari wazembe, ili watumbuliwe.

Dk. Mwakyembe amesema hayo baada ya kubaini uzembe unaofanywa na baadhi yao huku wakibweteka kukaa maofisini bila kufanya kazi.

Amesema maofisa habari wasiojituma ni sawa na kuwa na maofisa habari hewa, ambao wanakula mishahara wasiyoifanyia kazi, jambo ambalo hakubaliani nalo.

Alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa kazi wa siku tano wa maofisa habari, mawasiliano na uhusiano serikalini, unaofanyika jijini Arusha, aliwataka kubadilika na kutekeleza malengo waliojiwekea.

"Kweli naangalia tovuti za halmashauri zipo tisa tu zinazofanya vizuri, zingine wahusika wamelala; na mikoa 18 tu inafanya vizuri kuhabarisha, sasa hawa wengine wajitathmini vinginevyo nitapeleka majina yao kwa Waziri Mkuu, ili watumbuliwe, tutoe ajira kwa wengine," amesema.

Amewataka kufanye kazi ya kuhabarisha wananchi kazi zinazofanywa na serikali, ili wasitumbuliwe.

Amefafanua kuwa hata wizara yake pia wapo wazembe nao atapeleka taarifa zao ngazi ya juu ili wachukuliwe hatua, lengo ni kwamba kazi nzuri zinazofanywa na serikali zitambulike kwa wananchi na kuziba mianya kwa wapotoshaji wa taarifa za serikali.

Dk. Mwakyembe amewataka maofisa habari hao kujituma na kutoa taarifa za kazi zinazofanyika kila siku kwenye mitandao ya kijamii na endapo watazuiwa na mtu yeyote, wawafichue hata kwa siri ili wizara ishughulike na mhusika.

No comments:

Post a Comment