Wednesday, 14 March 2018

Serikali yaja na bajeti ya trilioni 32/-

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango

Mary Meshack, Dodoma

SERIKALI imewasilisha makadilio ya mapato na matumizi yake katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/19, ambapo inatarajia kukusanya na kutumia sh. trilioni 32.476 ikilinganishwa na trilioni 31.712 za mwaka uliopita huku matumizi kwa ajili ya maendeleo ikiwa ni  sh. trilioni 12.007 sawa na asilimia 37  ya bajeti yote.

Akiwasilisha mbele ya wabunge Mapendekezo ya Serikali ya Mpango  wa Maendeleo kwa mwaka huo wa fedha, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango amesema, mfumo wa ukomo wa bajeti hiyo ,umezingatia hali halisi ya upatikanaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali.

Amesema mapato ya ndani ikijumuisha ya halmashauri yanatarajiwa kuwa sh. trilioni 20.894 sawa na asilimia 64 ya bajeti yote.

“Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya kodi ya sh. trilioni 18.0 sawa na asilimia 13.6 ya pato la Taifa,” amesema Dk. Mpango

Ameongeza kuwa mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia sh. trilioni 2.158 kutoka vyanzo vya halmashauri itakusanya sh. bilioni 735.6.

Pia Dk.Mpango amesema,vyanzo vingine vya mapato ni pamoja na misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya sh. trilioni 2.676 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ikiwa ni asilimia nane ya bajeti yote.

"Serikali pia, inatarajia kukopa sh.trilioni 5.793 kutoka  soko la ndani ambapo nyingine sh. trilioni 4.6 ni kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva na sh. trilioni 1.193 ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo,

"Kiasi cha sh trilioni 1.193 ambazo ni mikopo mipya ni sawa na asilimia 0.9 ya Pato la Taifa na ili kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi muhimu ya miundombinu, serikali inatarajia kukopa sh. trilioni 3.111 kutoka soko la nje."

Kuhusu matumizi ya sh. trilioni 32.476 kwa mwaka 2018/19,Waziri huyo amesema, kati ya fedha hizo, sh. trilioni 20.468 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti .

“Matumizi  ya kawaida yanajumuisha sh. trilioni 10.004 kwa ajili ya kulipia deni la Serikali wakati  sh. trilioni 7.369 mishahara na nyingine trilioni 3.094 matumizi mengineyo (OC), na bilioni 389.9 ni kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya halmashauri,”amesema.
Matumizi ya maendeleo

Kwa upande wa matumizi ya maendeleo, Dk,Mpango amefafanua kuwa Serikali imepanga kutumia sh. trilioni 12.007 sawa na asilimia 37  ya bajeti ambapo kiasi hicho kinajumuisha sh. trilioni 9.876 sawa na asilimia 82.3 ni fedha za ndani na sh. trilioni 2.130 sawa na asilimia 17.7 ni kutoka nje.

Hata hivyo, Dk.Mpango amesemakiasi hicho cha fedha za maendeleo hakihusishi uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi, mashirika ya umma na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika ya umma na sekta binafsi ili kufanikisha kutekeleza miradi ya maendeleo.

Maoni ya wabunge

Wakitoa maoni kuhusu mpango huo wa maendeleo baadhi ya wabunge wameupongeza huku wakiitaka Serikali kuutekeleza kama ilivyopanga.

Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema, Serikali imejitahidi kuwa na mpango mzuri wa bajeti tofauti na miaka iliyopita.

"Serikali imejitahidi kuja na mpango mzuri,maana safari hii imegundua ukusanyaji wa mapato siyo mzuri na hivyo imejifunza kwa kuongeza kiasi cha takriban trilioni moja tu kutoka bajeti inayoishia Juni mwaka huu,” amesema Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), amesema, kinachohitajika katika mpango huo ni utekelezaji.

Kwa upande wake Mbunge wa Same Mashariki Naghenjwa Kaboyoka (Chadema), amesema mpango ni mzuri lakini usiwe wa kwenye makaratasi tu.

“Mipango katika makaratasi ni mizuri, lakini katika uhalisia bado hali si nzuri sana hususan katika maeneo ya vijijini, wananchi wanapata shida, barabara mbaya na uzalishaji unakuwa duni,” amesema mbunge huyo. 

Ameongeza kuwa katika mpango  huo, Serikali inapaswa kuzingatia kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua pekee.

Kaboyoka amesema,asilimia 37 iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo licha ya kuwa ni kidogo, Serikali ikitekeleza kama ilivyopanga, hali itakuwa nzuri.

Kwa upande wake Mbunge wa Kiembesamaki, Ibrahim Razar (CCM), amesema, kama Serikali itauelekeza mpango huo vizuri, ni dhahiri wananchi watanufaika nao.

No comments:

Post a Comment