Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, kulia kwake ni naibu wake, Anton Mavunde.
SERIKALI imesema
itaendeleza mapambano dhidi ya vita vya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi kwa
kuongeza kasi katika kuzuia maambukizi mapya ikiwemo kutoa elimu kwa
umma.
Akizungumza leo
mjini Dodoma wakati wa warsha kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
inayoshugulikia Ukimwi na dawa za kulevya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema dhamira ya Serikali
baada ya kuanzisha mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) ni kuhakikisha
kuwa mfuko huo unajengewa uwezo ili kutimiza lengo la kuanzishwa kwake.
“Tayari mfuko
umeweza kukusanya sh. bilioni 279 katika kipindi kilichopita na mwaka huu sh. bilioni
3 zimetengwa katika Bajeti na zitaingizwa katika mfuko huu ili uweze kutimiza
majukumu yake kwa ufanishi na tumekuwa tukiwashirikisha wadau kuchangia na
wamekuwa wakituunga mkono na tunaendelea kuwaomba wajitokeze zaidi kuchangia
mfuko huu,” amesisitiza Mhagama.
Akifafanua
Mhagama amesema tayari mapendekezo kuhusu kuwepo tozo maalum katika kodi
yameshawasilishwa katika kamati husika kwa hatua zaidi dhamira ikiwa ni
kuujengea mfuko huo uwezo wa kuwa na fedha za kutosha katika kufanikisha vita
dhidi ya Ukimwi hapa nchini.
Mkakati
mwingine ni ujenzi wa kituo maalum katika eneo la Mererani mkoani Manyara
kitakachosaidia katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kuwa eneo hilo ni moja ya
maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli za uchimbaji
madini.
Hatua nyingine
ni kufanya kazi kwa kushirikiana kati ya Tacaids na Mamlaka ya Kupambana
na Dawa za Kulevya ili kuwafikia waathirika wa dawa za kulevya ambao ni moja ya
makundi yanayoathika na ugonjwa wa Ukimwi kwa mujibu wa tafiti mbalimbali.
Kwa Upande wake
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Osca Mukasa amesema kutengwa fedha katika bajeti ya
2018/19 zitakazopelekwa katika mfuko wa kudhibi Ukimwi ni ishara nzuri kuwa
serikali imeweka mkazo katika mapambano dhidi ya janga hilo.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko amesema Tume hiyo iko katika
hatua za mwisho za kukamilisha mkakati wa Nne unaolenga kuongeza nguvu
ili kufikiwa kwa malengo ya mkakati huo.
Akifafanua Dk.
Maboko amesema tume hiyo imeandaa kampeni maalum za kuhamasisha wananchi kupima
ili kujijua kama wameambikizwa virusi vya Ukimwi au laa hali itakayowasaidia
kuchukua hatua stahiki na kwa wakati hivyo kuzuia maambukizi mapya hasa kwa
vijana.
“Hapa nchini kwa
mwaka kuna maambukizi mapya 81,000 hivyo ni vema tukaungana katika mapambano
dhidi ya ugonjwa huu kwa kuwa uwezo wa kuzuia maambuki mapya tunao”. amesisitiza
Dk. Maboko.
Warsha kwa
wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya imefanyika
mjini Dodoma leo ikiwashirikisha wajumbe wote wa kamati hiyo, Aidha mfuko
wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) unalenga kuongeza rasilimali fedha kutoka
asilimia 7 (2015) hadi asilimia 30 (2018).
No comments:
Post a Comment