Monday, 12 March 2018

Shahidi adai walikuta kipisi cha sigara nyumbani kwa Wema
Wema Sepetu

Mwandishi Wetu

KESI ya matumizi ya dawa za kulevya inayomkabili msanii Wema Sepetu imeendelea kusikilizwa leo katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es Salaam ambapo mjumbe wa shina eneo analoishi mshtakiwa huyo ametoa ushahidi dhidi ya tuhuma hizo.

Shahidi huyo, Steven Alphonce  amedai kuwa wakati wa upekuzi  ndani ya nyumba ya Wema kubaini iwapo kuna dawa za kulevya, alikuwepo (shahidi)   walikuta kipande cha sigara wala si bangi.

Alphonce amesema hayo mahakani hapo mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba akiongozwa na wakili wa serikali, Constantine Kakula.

Katika kesi hiyo inayomkabili Wema na wenzake wawili, shahidi huyo amedai alishiriki katika upekuzi nyumbani kwa Wema na kukuta kipande hicho cha sigara jikoni ambapo sehemu nyingine waliyopekua ni chumbani kwa Wema anakohifadhi viatu na nguo zake.

Shahidi huyo amedai kuwa bangi anaijua ikiwa shambani kwa kuwa alishawahi kuiona alipokuwa mkoani Shinyanga, lakini ikiwa nje ya hapo hawezi kuitambua.

Wema na wenzake wawili  wanashtakiwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi na walikamatwa Februari 4, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment