Tuesday, 6 March 2018

Simba 200 wanauawa kila mwaka nchini


Simba
ZAIDI ya simba 200 wanauawa na wafugaji wanaoishi pembeni mwa mbuga za wanyama na maeneo ya hifadhi kila mwaka hapa nchini.
Hiyo ni kwa mujibu wa mtafiti na mhifadhi kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania, Dk. Dennis Ikanda.
Dk. Ikanda ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kwamba kutokana na idadi ndogo ya simba iliopo hivi sasa ulimwenguni kote, kuna haja ya hatua madhubuti kuchukuliwa kukomesha migogoro kati ya wafugaji na wanyamapori.
Ongezeko la idadi ya mifugo na uhaba wa maeneo ya kulishia mifugo yao inawasukumua wafugaji wengi kwenda kutafuta malisho karibu na mipaka ya maeneo ya hifadhi.
Wafikapo huko, ndipo hukutana na simba na wanyamapori wengi ambao huwashambulia mifugo yao. Hivyo, simba wanaposhambulia wanyama wao, wafugaji pia wanawaangamiza kwa kuwaua.
Hata hivyo Dkt Ikanda anasema hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kwamba simba wako hatarini kutoweka siku za hivi karibuni.
“Tanzania ina idadi kubwa sana ya simba na hii ni kutokana na eneo kubwa lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa simba na wanyama wengine.
“Tunakadiria kwamba idadi ya simba ni kati ya 16,000 na 17,000 ambao wapo maeneo ya hifadhi ambayo yako mbali na wakulima. Kwa hivyo, tutaendelea kuwa na simba mradi tu mipaka ya hifadhi itatunzwa na kuheshimiwa,”  Dk. Ikanda amesema.
Hata hivyo, Dk. Ikanda amesema elimu zaidi ya hifadhi kuhusu umuhimu wa simba na wanyamapori kwa ujumla inahitajika kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi ili wafahamu mchango wao katika pato la taifa.
Amesema pia kuna haja ya kuwasaidia wakulima kupata vyanzo vingine vya mapato ili wasiendelee kutegemea mifugo tu kukidhi mahitaji yao ya kiuchumi.
Mbuga ya Ruaha iliyopo kusini mwa Tanzania inaaminika kuhifadhi takribani asilimia 10 ya idadi ya simba iliyopo duniani kote.


No comments:

Post a Comment