Tuesday, 13 March 2018

Theresa May: Jasusi alipewa sumu kali ya novichok

Sergei Skripal (66), na Yulia (33), wamo katika hali mahututi hospitalini
WAZIRI Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema jasusi wa zamani wa Urusi na binti yake walipewa sumu kali ambayo ni sehemu ya kundi la kemikali za sumu kwa jina Novichok.
Sergei Skripal na binti yake Yulia bado wamo katika hali mahututi hospitalini baada ya jaribio hilo la kuwaua eneo la Salisbury hapo Machi 4. Kemikali hiyo ilitambuliwa na wataalamu katika maabara ya ulinzi na sayansi Porton Down.
Novichok maana yake ni mgeni kwa lugha ya Kirusi. Ni jina linalotumiwa kurejelea kemikali za sumu ambazo zinashambulia mfumo wa neva mwilini. Kemikali hizo ziliundwa na Muungano wa Usovieti miaka ya 1970 na 1980.
Zilifahamika kama silaha za kemikali za kizazi cha nne na zilistawishwa chini ya mpango wa silaha za Muungano wa Usovieti uliofahamika kama "Foliant".
Mwaka 1999, maofisa wa ulinzi kutoka Marekani walisafiri hadi Uzbekistan kusaidia kuvunja na kusafisha moja ya eneo kubwa zaidi lililotumiwa kufanyia majaribio silaha za kemikali na Muungano wa Usovieti.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa ngazi za juu ambaye alitorokea Marekani, maofisa wa Usovieti walitumia kiwanda kilichokuwa eneo hilo kuunda na kufanyia majaribio sampuli za kemikali ya Novichok. Kemikali hii iliundwa mahsusi kutoweza kugunduliwa na wakaguzi wa silaha na sumu katika mataifa mengine.
Moja ya kemikali hizi zinazofahamika kama Novichok - A-230 - inadaiwa kuwa na nguvu mara 5-8 zaidi ya sumu nyingine hatari kwa jina VX.
"Hii ni sumu hatari na changamano kushinda sumu aina ya sarin au VX na pia huwa vigumu zaidi kuitambua," anasema Prof Gary Stephens, mtaalamu wa kemikali katika Chuo Kikuu cha Reading.
Sumu ya VX ndiyo iliyotumiwa kumuua ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un mwaka jana, kwa mujibu wa Marekani.
Aina mbalimbali za kemikali hii ya A-230 zimekuwa zikitengenezwa, na aina moja inadaiwa kuidhinishwa na jeshi la Urusi itumike kama silaha ya kemikali.
Ingawa baadhi ya aina za sumu hii ya Novichok huwa majimaji, kuna aina nyingine ambazo ni yabisi (gumu au isiyokuwa majimaji).
Ni kemikali ambayo pia inaweza kugeuzwa kuwa poda laini.
Baadhi ya sumu hizi pia hudaiwa kutumiwa kama "silaha za ngazi mbili". Hii ina maana kwamba sumu hii huhifadhiwa mara nyingi kama kemikali aina mbili ambazo zikiwa kando kando si hatari. Zinapochanganywa, huingiliana na kutengeneza sumu.
Hii huifanya rahisi sana kwa viungo vya kemikali hii kusafirishwa kwani huwa sumu tu zikichanganywa.
"Moja ya sababu ambayo hufanya sumu hizi kuandaliwa ni kwa sababu viungo vyenyewe havijapigwa marufuku, Hii ina maana kwamba kemikali hizi ambazo huchanganywa huwa rahisi kusafirishwa bila kuwa hatari kwa anayezisafirisha," anasema Prof Stephens.
Mtu anapopumua sumu ya Novichok, au hata ikigusa ngozi yake, basi huanza kumuathiri upesi. Dalili zake zinaweza kuanza kujionesha katika kipindi cha muda mfupi hivi, sekunde 30 hadi dakika mbili.
Hata hivyo, sumu hii ikiwa kama poda huchukua muda zaidi kuanza kuathiri mtu.Dalili kali zinaweza kuanza kujionesha saa 18 baada ya mtu kukumbana na sumu hiyo.
Chanzo:BBC

No comments:

Post a Comment