Friday, 23 March 2018

Tizeba ataka majina ya waliohusika sakata la korosho za kokoto yafikishwe kwa IGPDk. Charles Tizeba

Peter Simon

WAZIRI wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, ameagiza kuwasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), orodha ya watu wote waliohusika katika sakata la korosho za Tanzania zilizokutwa na kokoto nchini Vietnam ili wakamatwe na kuhojiwa.
            
Hata hivyo, amesema taarifa zinasema jambo hilo si la kwanza kufanyika nchini. Ametoa agizo hilo jana baada ya kuwasilishwa taarifa ya uchunguzi wa korosho hizo iliyotolewa na kamati iliyoundwa kuchunguza suala hilo.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Dk. Tizeba amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mathew Mtigumwe, kuwasilisha orodha hiyo kwa IGP ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.

“Waende sasa wakahojiwe rasmi na vyombo vya dola, naomba hili lifanyike leo (jana) ili wahojiwe kwamba wewe fulani ulikuwa mahali fulani wajibu wako ulikuwa huu hukufanya hivyo, na kama wakibainika wana kesi ya kujibu sheria ichukue mkondo wake,” amesema Tizeba.

Amesema katika ripoti hiyo kuna majina ya watu waliohusika katika kusimamia shughuli yote ya usafirishaji wa korosho kuanzia ziliponunuliwa, kampuni ya usafirishaji, waliofanya ubadilishaji kwenye shirika la meli nchini (Nassaco).

“Majina yao yamo na Ofisa wa Serikali wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aliyetakiwa aweke ‘seal’ kwenye hizo kontena kwa wakati baada ya kuwekwa kwenye magunia ili kujiridhisha kwamba alichokishuhudia kinawekwa kwenye kasha hakitabadilishwa na kuweka lakiri ya serikali kwamba humo ndani kuna mzigo uko ndani ya udhibiti wa forodha, huyu naye anafahamika kwa jina,” amesema.

Amefafanua kuwa kwanini baada ya kufungwa makontena hayo yalibaki kwa muda wa siku tano hadi sita yawezekana hakukuwa na meli ya kusafirisha, lakini yale ya kusafiri yanakwenda yanapata nafasi kampuni ya kimataifa ya kuhudumia shehena za makontena Bandarini (TICTS), ambapo makontena ambayo yamefika huwa yanatoka kupisha yanayosafirishwa.

“Tutajua huyu naye ni nani ambaye pia yumo humu ambaye alitakiwa kuyatoa Nassaco kuyapeleka Ticts na TPA (Mamlaka ya Bandari), tutataka tujue hayo mambo nyie haikuwa kazi yenu kuchukua hatua, kazi yenu ilikuwa ni kukusanya taarifa,” amesema Tizeba.

Ameongeza kuwa ubalozi wa Vietnam ulifikisha serikalini malalamiko rasmi kuhusu mawe yaliyopatikana kwenye viroba vya korosho nchini humo.

“Mimi binafsi niliongea naye na akanionesha jinsi wafanyabiashara wa Vietnam walivyokuwa wamepokea korosho zilizochanganyika na vitu mbalimbali ikiwamo mawe,” amesema Tizeba.

Ameleza kuwa taarifa ya Balozi iliyoonesha korosho imenunuliwa mkoani Lindi, lakini akitazama mawe yaliyokuwamo sio ya Nachingwea au Liwale kunakopatikana mwambao wa pwani.

Amebainisha pia jambo jingine ambalo limeendelea kujitokeza ni kuwapo mchanga kwenye magunia ya korosho na siku nne zilizopita imegundulika kontena moja lilikuwa limechanganywa na mawe katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dk. Tizeba amesema mtu amenunua tani 20 za Korosho zinaondolewa tani 3 au 1.5 badala yake yanaingizwa mawe au mchanga na michikichi.

Amesema atampa ripoti hiyo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ili aweze kuona mambo yanayohusu wizara anayosimamia na kama kuna uwezekano wa kuboresha.

“Pia taasisi zingine za serikali zinazohusika na masuala hayo ambapo kuna maghala yanayosimamiwa na Wizara ya viwanda na biashara nitampa hii ripoti Charles Mwijage,” amesema.

Amesema kwa upande wa serikali wanaendelea na jitihada kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na kwamba leo au kesho watakutana na wabunge kutoka Vietnam.

“Tutakutana nao tuzungumze hili suala la korosho tuliweke vizuri, tumekutana na Balozi ambaye kasema wabunge hao wapo nchini na wangependa na wao kusikia.Tulikuwa tunasubiri ripoti yenu ilituwape picha kamili,” amesema.

No comments:

Post a Comment