Monday, 5 March 2018

TRA Dodoma yaonywa kuacha 'kuburuza miguu'
Profe. Davis Mwamfupe

      Mary Mechack, Dodoma

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), mkoa wa Dodoma imetakiwa kuongeza kasi ya kukusanya mapato stahiki ya serikali.

Akihutubia kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Dodoma mjini hapa leo katika uzinduzi wa wiki ya elimu kwa mlipa kodi,  meya wa manispaa ya Dodoma, Profe. Davis Mwamfupe amesema, mapato katika mkoa huo kwa sasa bado hayakidhi mahitaji  licha ya kuwa yanaongezeka mwaka kwa  mwaka.

“Hii ina maana kuwa wakati tunatambua mafanikio yaliyofikiwa, tunatakiwa kupiga hatua nyingine zaidi ili kuhakikisha mapato yanaendelea kuongezeka ili kutuwezesha kupunguza kiasi cha utegemezi wa misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali,”amesema.

Ameongeza kuwa wakati wa maadhimisho hayo ya wiki ya mlipa kodi ni wakati mwafaka wa kuweka mikakati ya kuhakikisha maeneo yote yanayopaswa kulipa kodi yanatekeleza wajibu wake.

“Pia huu ni wakati wa kuangalia mapungufu yaliyopo katika uhusiano baina ya mlipa kodi na TRA katika kutekeleza wajibu wa kukusanya kodi ili kuyarekebisha mapungufu hayo na kukuza ulipaji kodi wa hiyari, ”amesisitiza

Awali  meneja wa mkoa wa Dodoma, Thomas Masese alisema,TRA mkoani hapa inakabiliwa na changamoto  mbalimbali ikiwemo, baadhi ya walipa kodi kutokuwa na utamaduni wa kufanya hivyo kwa hiari.


No comments:

Post a Comment