Wednesday, 28 March 2018

TRA yazindua utoaji vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo


Kamishna mkuu wa TRA Charles kichere akizungumza wakati wa uzinduzi huo

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na wamachinga.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Kichere amesema utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo unatokana na marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambayo yanalenga kuwatambua wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.

“Baada ya marekebisho ya Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, zoezi hili la kuwatambua wafanyabiashara wadogo lilianza kutekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) pamoja na Idara ya Uhamiaji”, amesema Kichere.

Kichere amesema kwamba, TRA  kwa kushirikiana na wadau hao, ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa Kariakoo, Dar es Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo jana baadhi yao wamepatiwa vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo.

Ameongeza kuwa mchakato wa kutambua vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo na kuwapatia Kitambulisho cha Taifa na Namba ya utambulisho wa mlipa kodi unaendelea kufanyika nchi nzima na kubainisha kuwa ili wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo maalum,  wanatakiwa kujiunga katika vikundi vinavyotambuliwa kisheria na Serikali, kuwa na Kitambulisho cha Taifa, kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ya kikundi alichojiunga nacho pamoja na kuchangia sh. 10,000.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogo ili waweze kupiga hatua kiuchumi kutoka daraja la chini hadi la kati na hatimaye kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali.

“Lakini kwanza naomba nimshukuru  Rais wetu John Magufuli kwa hii ndoto yake ya kuwasaidia wanyonge waliokuwa wanafanya biashara ndogo ndogo kutambulika na Serikali na kisha waondoke katika hali ya daraja la chini na kufikia daraja la kati.  Nafurahi kuwaeleza kwamba, ndoto ya  Rais wetu imetimia”, amesema Mjema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo Dar es Salaam, Steven Lusinde amesema wamefurahishwa na azma ya Serikali ya kuwatambua wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi kwa kuwa wamekuwa na hamu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.

Moja ya majukumu ya TRA ni kukusanya mapato ya Serikali pamoja na kutoa elimu kwa walipakodi na watanzania ili kuongeza uhiari wa ulipaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yanahitajika katika kuleta maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment