Friday, 9 March 2018

Trump akubali kukutana na Kim Jong Un


Rais wa Marekani, Donald Trump (kushoto) na wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
RAIS wa Marekani, Donald Trump amekubali ombi la Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un la kutaka wakutane mapema ndani ya mwezi mei mwaka huu.
Hatua hiyo itakuwa ni ya kihistoria baada ya kutokuwepo rais wa Marekani ambaye amewahi kukutana na kiongozi mkuu wa Korea kaskazini.
Hata hivyo, mahala watakapokutana viongozi panabaki kuwa siri kwa sasa na pia Marekani imesisitiza kuwa pamoja na kukubali ombi hilo la Rais Kim Jong Un bado vikwazo vitasalia pale pale.
Tangazo hilo la kwamba Rais Trump amekubali kukutana na Kim Jong Un limetolewa na uongozi wa juu wa Korea Kusini uliokwenda mjini Washington kuwasilisha barua ya ombi hilo kutoka kwa Korea Kaskazini.
Kim pia amekubali kusitisha mpango wake wa nyuklia na majaribio yake ya makombora msimamo ambao ni tofauti na aliokuwa nao rais huyo hapo awali.
Hatua ya Rais Kim Jong Un kulegeza msimamo ni matokeo ya mazungumzo mazito yaliyofanywa wiki chache zilizopita baina ya ujumbe wa Korea Kusini na kiongozi huyo.

No comments:

Post a Comment