Tuesday, 20 March 2018

Trump apendekeza adhabu ya kifo dhidi ya walanguzi wa mihadarati

 Donald Trump
RAIS wa Marekani, Donald Trump amesema anataka kuweka adhabu kali ikiwemo ya kifo kwa wale watakaobainika kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, lengo ilikiwa ni kukabiliana na ongezeko kubwa la watumiaji nchini mwake.
Katika hotuba yake aliyoitoa akiwa New Hampshire, amesema wauzaji wa dawa za kulevya wamesababisha vifo vya maelfu ya watu, lakini cha ajabu baada ya kuhukumiwa kufungwa wanakaa muda mfupi tu gerezani jambo ambalo haliridhishwi nalo.
Ameongeza kuwa tatizo hilo linaweza kuondolewa kwa kutumia akili na kuwa imara pamoja na kutenga fedha.
“Mwezi oktoba tulitangaza tatizo hili kama janga la dharula kiafya ambalo limedumu kwa muda mrefu tangu kipindi kilichopita.Tumelifanyia kazi na bunge kuhakikisha tunatenga dola bilioni sita katika bajeti mpya ya mwaka 2018/2019 ili kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya,ambapo tutakuwa tumetenga kiasi kikubwa cha fedha kuwahi kutokea dhidi ya tatizo hili'.
Hata hivyo, Rais Trump ameelezea mikakati iliyowekwa tayari katika kukabiliana na dawa za kulevya hadi sasa.
“Kwanza kabisa tunapunguza kiwango cha uhitaji wa dawa hizo, kuhakikisha tunapunguza idadi ya watu wanaojiingiza na hatimaye kutekwa na matumizi ya dawa za kulevya.
“Ni muhimu sana. Hiyo inahusisha serikali kutoa fedha kwa ajili ya miradi isiyo jihusisha na masuala ya dawa za kupunguza maumivu na kuhamasisha matumizi ya dawa za kuondoa maumivu zisizo na madhara.
“Na ni jambo lililo ndani ya uwezo wetu.Lakini pia tunatoa ushauri na idara yetu inaliangalia suala hili kwa makini ikiwemo kuchukua hatua za kisheria,na tutalisimamia katika hatua ya kiserikali,” amesema.
Rais Trump ameahidi kujenga taifa huru katika masuala ya matumizi ya dawa za kulevya kwa kizazi kijacho na kuhakikisha hakuna mazingira yatakayosababisha watu kujitumbukiza katika matumizi yake. 

No comments:

Post a Comment