Saturday, 10 March 2018

Trump aweka masharti mkutano na Kim

Sarah Sanders

MKUTANO kati ya rais wa Marekani Donald Trump na Kim Jong Un wa hautafanyika hadi pale kiongozi huyo wa Korea kaskazini atakapochukua hatua thabiti, Ikulu ya Marekani , White House imesema.

Kukubali  kwa  Trump  mwaliko  wa  Kim kukutana naye, bila  masharti  ya  awali, kumekuja  kwa mshituko kwenye sehemu kubwa  ya  jumuiya  ya  kimataifa kwa kuwa hakuna  rais  wa  Marekani aliyeko  madarakani  aliyekutana na  kiongozi wa  taifa  hilo  lenye usiri.

"Mkutano  huu  hautafanyika  hadi  pale  tutakapoona hatua  kamili ambazo  zinakwenda  pamoja  na  maneno  na malumbano  ya  Korea kaskazini," mkuu  wa  masuala  ya  mawasiliano  wa  Ikulu  ya Marekani White House Sarah Sanders  amesema.

Sanders  amedokeza  kwamba  Marekani haijafanya maridhiano yoyote na  Korea  kaskazini , wakati  Korea  kaskazini imetoa  ahadi kubwa za   kuachana  na  mpango wake  wa  kinyuklia na kuachana  na  hatua  yake  ya  kufanya  majaribio  ya  makombora na  kukubali  kwamba  luteka ya  kila  mara  ya  kijeshi  kati  ya Marekani  na Korea  kusini itaendelea.

Trump ana matumaini kwamba  hatua  zaidi  zinaweza  kupigwa, Sanders amesema na  kwa  wakati  huu, Marekani  haitaacha kuendelea  kuweka  mbinyo  dhidi  ya  Korea  kaskazini  ili  kufikisha mwisho  mpango  wake  wa  kinyuklia. Jioni  ya  jana  Ijumaa  Trump amesema , makubaliano  yako  "karibu  sana kupatikana."

"Makubaliano  hayo  na  Korea  kaskazini  yanatayarishwa  na yatakuwa , kama  yatakamilika, mazuri  sana  kwa  dunia," Trump aliandika  katika  ukurasa  wake wa  Twitter, akimaanisha  kwamba  Korea kaskazini  inaachana  na  silaha  zake  za  kinyuklia. "Muda  na mahali  pataamuliwa," aliongeza.

Mkutano  baina  ya  kiongozi wa  Marekani  na  Korea  kaskazini unaweza  kuwa  fursa  ya mafanikio  katika  miongo kadhaa  ya juhudi  za  kurejesha  amani  katika  rasi  ya  Korea.

Mualiko  wa Kim  unafuatia hatua  kadhaa  za  kidiplomasia , zinazoonekana  na  wachunguzi  wengi  na  vyombo  vya  habari kuwa  kama "hatua  za kuvutia" zilizounganishwa  na  kuhudhuria kwa  Korea  kaskazini  katika  mashindano  ya  olimpiki  ya  majira ya  baridi mjini  Pyeongchang mwezi  uliopita.

Chung Eui Yong, ambaye  aliongoza  ujumbe  wa  Korea  kusini  kukutana  na  na  Kim mjini  Pyongyang mapema  wiki  hii, alikuwa  wa  kwanza  kutangaza kukubali  kwa  Trump mwaliko  huo.

Kiongozi  wa  Korea  kaskazini , alieleza "kuwapo  kwake  tayari " kukutana  na  Trump, na  Trump atakutana  na Kim  mwezi  Mei "ili kufanikisha kuondolewa  kwa  silaha  za  kinyuklia  kabisa;" Chung aliwaambia  wanahabari.

Maafisa  wa  Korea  kusini walifikisha  mwaliko  huo  kutoka  kwa  Kim siku  ya  Alhamis wakati walipouarifu  utawala  wa  Trump  kuhusiana  na  mazungumzo  ya hivi  karibuni  kati  ya  Korea  mbili.

Licha  ya  wachambuzi  wengi  kuona  hatua  hizo  kama  ni mabadiliko  ya  kushangaza, waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa Marekani Rex Tillerson  amesema  Trump  kukubali  mwaliko , "sio jambo  la  kushangaza bila  shaka." Ripoti  kutoka  kwa  Wakorea kusini zinaonesha "hamasa kubwa " kutoka  kwa  Kim  kutaka kuzungumza  na  Marekani, Tillerson  amesema.

Chanzo: DW


No comments:

Post a Comment