Donald Trump
RAIS wa Marekani, Donald
Trump ametangaza mpango wa ongezeko la ushuru wa forodha kwa bidhaa za China.
Hali hiyo
inatarajiwa kuongeza vita vikali vya kibiashara ambavyo huenda vikawa na
madhara kwa mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani.
Hata hivyo, Trump ametia saini hati ya
maelekezo kwa maofisa juu ya namna ya kushughulikia suala la ushuru kwa bidhaa
za mabilioni ya dola zinazoingizwa kutoka nchini China.
Trump amesema awali aliiona China kama rafiki,
lakini amebaini kuwa vikwazo vinahitajika baada ya kugundua kuwa taifa hilo linaonekana
kutaka kujinufaisha kijanja katika uendeshaji biashara ambao umekuwa ukiingizia
Marekani hasara ya mabilion ya dola kila mwaka.
Amesisitiza kuwa China ni moja kati ya mataifa
anayokusudia kuingia katika majadiliano ya kibiashara.
"Ndiyo tumeanza majadiliano
na Umoja wa Ulaya, kwa sababu wametuwekea vikwazo, kuna mazingira ambayo
yanawaruhusu kufanya biashara na sisi, lakini sisi hatuwezi kufanya biashara na
wao.Wana vikwazo vikubwa dhidi yetu,wana ushuru wa forodha mkubwa sisi
hatuna,siyo haki.
“Nao Nafta wamekuwa wabaya kwetu, lakini
tutajitahidi kurekebishana ama kufanya kitu cha ziada. Mpango wa kibiashara na
Korea Kusini ni wa upande mmoja, unatakiwa kufanyiwa mabadiliko.
"Kwa hiyo kuna
mambo mengi yanayotokea, lakini kwa suala la China tutatumia kifungu 301
ambacho kitahusisha dola bilioni 60
ambazo ni sehemu tu ya hiki tunachokizungumza,”amesema Trump.
Hatua hii ya rais Trump dhidi ya China imekuja
baada ya uchunguzi wa mwezi Agosti mwaka jana kuhusu suala la forodha ambao
uliagizwa kufanyika na Trump mwenyewe.
China kwa upande wake imeonya na kuongeza kuwa
iko tayari kujibu mashambulizi ya kibiashara dhidi ya Marekani na imeituhumu
Marekani kwa kukiuka sheria za kimataifa za kibiashara.
No comments:
Post a Comment