Thursday, 22 March 2018

Trump kutangaza vikwazo dhidi ya China baada ya uchunguzi


Donald Trump 

RAIS wa Marekani, Donald Trump anatarajiwa kutangaza vikwazo dhidi ya China leo Alhamis baada ya kubaini taifa hilo linashinikiza wizi na uhamisho wa ubunifu kutoka biashara za taifa hilo kubwa duniani.
Ikulu ya White House imesema hatua hiyo inajiri baada ya miaka kadhaa ya mazungumzo yaliyoshindwa kupata suluhu kuhusu suala hilo. Vikwazo hivyo vitashirikisha ushuru na masharti mengine.
Mpango huo umezua hofu kuhusu vita vya kibiashara. Ikulu ya White House imeripotiwa na vyombo vya habari vya Marekani kuweka ushuru wa kati ya $30bn-$60bn kwa mwaka pamoja na masharti ambayo yatazuia uwekezaji .
Vilevile huenda Marekani ikawasilisha malalamiko yake kwa shirika la biashara duniani WTO, kulingana na maofisa wa biashara. Mpatanishi mkuu wa biashara nchini Marekani Robert Lighthizer amewaambia wabunge wa Congress siku ya Jumatano kwamba Marekani inafaa kuiwekea China shinikizo kali. Lighthizer amesema kulinda ubunifu ni muhimu kwa uchumi wa Marekani.
''Ni suala muhimu sana'' , amesema Lighthizer. ''Nadhani kitakuwa kitu muhimu ambacho kitafanyika ili kuleta usawa wa kibiashara''.
Ofisa biashara nchini Marekani ambaye alizungumza na wanahabari amesema nchi yake ina ushahidi kwamba China inataka kampuni za Marekani kuingia katika ushirikiano na kampuni za China ili kuingia katika soko la taifa hilo kwa lengo la kuzishinikiza kampuni hizo kuhamisha teknolojia yao.
Marekani pia iligundua kwamba China inawekeza katika kampuni muhimu za Marekani na kufanya mashambulio ya mitandao. Matokeo hayo yanatoka katika uchunguzi ulioagizwa na rais Trump Agosti mwaka jana kwa jina 301.
Katika kipengee cha 301 cha sheria ya biashara, serikali imejipatia uwezo wa kuwekea vikwazo mataifa ambayo inahisi hayafanyi biashara kwa usawa. Trump mara kwa mara amekuwa akilalamika kuhusu ukosefu wa usawa kibiashara kati ya Marekani na China.
Kuna wasiwasi mkubwa nchini Marekani kwamba China inatafuta teknolojia ambayo wanaweza kuitumia kijeshi. Bunge la Congress pia linapanga kupitisha sheria ambayo itaipatia serikali uwezo wa kubadilisha mikataba ya biashara za kigeni kutokana na vitisho vya kununua viwanda vya Marekani.
Lakini wanasiasa na viwanda ikiwemo watumiaji wameonesha wasiwasi kwamba huenda China ikalipiza kisasi. Lighthizer amesema kuna uwezekano mkubwa wa China ikalipiza kisasi akidai kwamba Kilimo cha Marekani huenda kikaathiriwa , lakini akasisitiza kwamba hatua hiyo haitaizuia Marekani kuchukua hatua.Iwapo watalipiza kisasi basi Marekani italazimika kuwalinda wakulima wake.

China imesema hakutakuwa na mshindi  katika vita vva kibiashara. Siku ya Jumanne ambayo ni ya mwisho ya kikao cha kila mwaka cha chama tawala cha taifa hilo, kiongozi wa China Le Keqiang amesema ombi lake ni kwamba pande zote mbili zinafaa kutulia.
Pia amesema anatumai Marekani itapunguza masharti kuhusu bidhaa za kiteknolojia zinazoingia China.

No comments:

Post a Comment