Wednesday, 28 March 2018

TTCS yatumia milioni 400/- kujenga ofisi za vijiji


Meneja Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), Leonard Charles akimuonesha Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Adam Mgoi (kushoto), mti wa Myombo uliokuwa umekatwa kwa ajili ya mkaa mwaka mmoja uliopita na sasa umestawi, (kulia) ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kessy Mkambala (PICHA NA SULEIMAN KASEI).

Suleiman Kasei, Morogoro

MRADI wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa (TTCS), umetumia sh. milioni 420 kwa ajili ya kujenga ofisi 12 za vijiji mbalimbali vilivyopo katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro Vijijini mkoani Morogoro.

Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa TTCS, Leonard Charles wakati akizungumza na mwandishi wetu, katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kijiji cha Kitunduweta wilayani Kilosa ambacho kimejengewa ofisi ya kijiji.

Meneja amesema kila ofisi imegharimu sh. milioni 35 ambazo zimegawanywa katika ofisi tatu, ukumbi na mahabusu ambayo yanatumika kwa majukumu ya Serikali ya kijiji.

“Katika ofisi hizi kunakuwepo ofisi ya mtendaji wa kijiji, mwenyekiti wa kijiji, ofisi ya maliasili, ukumbi na mahabusu na hii ni ramani ya kila tunapotekeleza mradi,” amesema.

Ameongeza kuwa pamoja na ujenzi huo pia wanawapatia thamani za ndani ili viongozi hao waweze kufanya kazi katika hali nzuri.

Charles amesema wanalazimika kujenga ofisi za vijiji ili kuwarahisishia wao kufanyakazi kwa karibu na wanavijiji na serikali zao na kurahisisha kutekelezeka mradi kwa haraka.

Amesema kupitia ofisi hizo kamati ya maliasili ya kijiji imekuwa na uwezo wa kusimamia mradi kwa kuwa na ofisi ya kufanya kazi zake bila kupata bughudha huku ushirikiano mkubwa kutoka ofisi ya kijiji ukiwepo.
Tumetumia zaidi ya sh. milioni 400 kujenga ofisi za vijiji 12 vya Msimba, Msanga, Mhongwe, Kitunduweta, Mhendaa, Mlilingwa, Viguzi, Matuli na Lilongwe na hili tunalifanya ili kuleta ufanisi wa mradi,” amesema.

Aidha, meneja huyo ameongeza kuwa wanajiandaa kufanya tathmini ya mradi ambayo itashirikisha halmashauri ambao ni wadau wakubwa katika utekelezaji wa mradi huo kupitia kata zao na vijiji vilivyopo ndani ya mradi.

Charles amesema pamoja na tathmini hiyo wanayotarajia kuifanya wanaiomba halmashauri kuanza kusambaza mradi huo katika vijiji mbalimbali ambavyo vina sifa ya kupokea mradi kama huo ili mpango huo uende kwa kasi.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo, Adam Mgoi amelitaka Baraza la Madiwani kuteua kijiji cha mfano ili iweze ili kuanzisha na kufadhili mradi unaohamasisha wananchi kulinda misitu yao unaojulikana zaidi kama mkaa endelevu.

Ameitaka halmashauri ijielekeze katika maeneo ambayo ni hatari kwa uharibu wa misitu hususan maeneo ya Kaskazini mwa wilaya ya Kilosa, kuanzia eneo la Mbaku, Kwambe na vijiji vingine ambavyo vitaonekana kuharibika.

“Ili kuunga mkono jitihada za TTCS, mwaka ujao, halimashauri itakuwa na kijiji ambacho na wao watakifanya kama kijiji cha mfano kwa sababu tuna walimu wa kutosha kutoka vijiji 20 vilivyopo kwenye mradi,” amesema.

Mgoi amesema pamoja uanzishaji wa kijiji cha mfano amevitaka vijiji vinavyotekeleza miradi kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuongeza mapato ili kusaidia Serikali kuleta maendeleo.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Margaret Magele, alisema mradi huo umechangia katika kukiwezesha kijiji kujenga ofisi ya kisasa, kukarabati madarasa mawili na ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambayo imefikia hatua za mwisho kukamilika.

No comments:

Post a Comment