Tundu Lissu
Suleiman Kasei
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (Chadema), amewataka maaskofu, mashekhe, wachungaji, mapadri, wainjilisti,
maimamu na wananchi kwa ujumla waamke kulaani vikali vitendo anavyodai vya
ukandamizaji wa haki za binadamu.
Lissu ameyasema hayo ikiwa ni siku
chache baada ya Mchungaji wa Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Dayosisi ya Kilimanjaro Kati, Fred Njama kuhojiwa na Jeshi la Polisi
mkoani humo.
Pamoja na Jeshi la Polisi kutosema
sababu za kumkamata Mchungaji Njama, tukio la kukamatwa na kuhojiwa kiongozi
huyo linakuja ikiwa ni siku chache baada ya kutoa taarifa ya kanisa lake kwa waamini
ambapo aliaonisha changamoto mbalimbali zilizopo nchini kwa sasa.
Kwa mujibu wa video ambayo imesambaa
mitandaoni ikimuonesha Mchungaji Njama anasema uchumi haujaimarika na umaskini
unaendelea kuongezeka kwa nguvu.
“Umaskini umendelea kuongezeka kwa
nguvu, tumeshuhudia biashara nyingi zikifungwa, wakulima wamekata tamaa na
gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa sana,” amesema.
Pia mchungaji huyo ameongeza kuwa serikali
haitoi ruzuku ila wakati wa kuuza mazao wakulima hawana uhuru wauze wapi kwa
bei gani, wafugaji pia wanazalisha kwa gharama kubwa.
Akizungumzia hali hiyo Lissu amesema
kwa matukio ambayo yametokea takribani miaka miwili sasa ni wazi kuwa kila
mwanajamii anapaswa kunyanyuka na kuachana na dhana ya kundi fulani kwani yote
yameguswa.
“Maaskofu, wachungaji, mapadri,
wainjilisti, mashehe, maimamu na kila aina ya kiongozi wetu wa kidini, waamke
na kulaani vikali vitendo hivi vya ukandamizaji wa haki za binadamu za viongozi
wa kiroho kutoa maoni yao hadharani na kukemea maovu ya utawala huu,” amesema.
Amefafanua kuwa ni wakati sasa wa waumini
wao kuunga mkono na kushikamana nao na vyama vyetu vya siasa, taasisi za kiraia
na kitaaluma na vyombo vya habari, navyo vipige kelele.
“Kelele ya umma dhidi ya ukandamizaji
ni kelele ya Mungu. Kimya mbele ya ukandamizaji ni kuunga mkono ukandamizaji,”
amesema.
Amefafanua kuwa pamoja na ukweli
kwamba aliyekamatwa ni kiongozi wa kidini, lakini sio viongozi wa kiroho
peke yao wanaotakiwa kulaani ukandamizaji wa aina hii wa haki za binadamu na
kuwa ni jambo la kila mmoja wetu.
Mbunge huyo amesema haki za binadamu
ni za watu wote pamoja na viongozi wa kidini na ukandamizaji wa haki hizo kwa
mtu mmoja ni ukandamizaji wa haki hizo kwa watu wote.
Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji kwa
matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma
na watu wasiojulikana amesema ni miaka miwili iliyopita alisema hali hii inapaswa
kupingwa na kila mwenye akili timamu lakini inawezekana hakueleweka.
“Tangu niyaseme maneno haya
mahakamani Kisutu Juni 29 mwaka 2016, ni watu wangapi wameuawa, kupotezwa,
kuumizwa, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya 'uchochezi' au mengineyo ya
ajabu ajabu,” amehoji.
Amesema ni watu wangapi wamepoteza
ajira zao, makazi yao, mali zao nyingine kutokana na matumizi ya ovyo ya
madaraka ya utawala ulioko madarakani.
Kwa upande wake Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam
Tanzania, Sheikh Rajab Katimba amesema kuna mahali taifa limekengeuka hali
ambayo inatoa picha mbaya kwa jamii.
Katimba amesema viongozi wa Serikali
wanapaswa kukaa na viongozi wale wa dini kuhakikisha jitihada za kusukuma
gurudumu la maendeleo zinafanyika kwani kuwepo kwa mazingira ambayo yanaonekana
kwa sasa sio afya nzuri kwa nchi.
“Tunatakiwa kukaa na kutafakari
kinachoendelea nchini kwa sasa haya ambayo yanatokea sasa sio tamaduni zetu
naamini tunapaswa kubadilika kwa maslahi ya Tanzania na Watanzania,” amesema.
Ameongeza kuwa viongozi wa dini na
Serikali wanapaswa kufanya kazi pamoja kinyume cha hapo Taifa litaenda
kusikohitajika kwani heshima ya viongozi wa dini inatakiwa kubakia pale pale.
Mwenyekiti wa jumiya hiyo Sheikh
Mussa Kundecha, amewataka viongozi kutambua kuwa hakuna mtu mkamilifu hivyo
wawe tayari kukosolewa pale inapobidi.
Kundecha amesema iwapo kila kiongozi
ataishi katika misingi hiyo hakuna ambaye ataona kuwa ananyimwa raha na upande
wowote huku akivitaka vyombo vya habari kutenda haki katika kuelimisha jamii.
Mtume Onesmo Ndegi, wa Kanisa la Living Waters Centre jijini Dar es Salaam, amesema
taarifa hizo amezisikia ila hajapata undani wake na kwamba anataka kuzifanyia
kazi ili aweze kuzungumza katika haki bila kumtuhumu mtu au taasisi.
No comments:
Post a Comment