Friday, 2 March 2018

Ushuru wa bidhaa za chuma wazua utata baina ya Trump, wafanyabiashara

Viwanda vya chuma vya Ulaya

WASHIRIKA  wakubwa wa biashara wa Marekani wamekasirishwa na tangazo la Rais wa nchi hiyo, Donald Trump kuhusu mpango wa kutoza ushuru kwa bidhaa za chuma na aluminiam zinazoingizwa.

Umoja wa Ulaya na Canada kwa pamoja wamesema watafanyia kazi uamuzi huo, kupingana na tamko hilo.

Rais wa Tume ya Ulaya Jean Claude Juncker amesema uamuzi huo wa Marekani wa kutoza ushuru utahatarisha maelfu ya kazi barani Ulaya.

Nchi za Mexico, China na Brazil wanasema wataziangalia hatua za kulipiza kisasi.

Trump aliweka ujumbe katika akaunti yake ya Twitter na kusema Marekani ilikuwa imekumbwa na "sera mbovu na zisizo sawa za kibiashara".

Amesema bidhaa za chuma zinazo ingizwa zingetozwa ushuru wa asilimia 25 na aluminiam asilimia 10.

Lakini wakosoaji wake wamesema shuru hizo hazitafanikiwa kulinda ajira za Marekani na hatimaye zingepandisha bei za bidhaa kwa wanunuzi.

Habari ziliathiri hisa za Asia ambazo zilishuka siku ya Ijumaa, huku hisa ya Japan, Nikkei ikipoteza zaidi ya asilimia 2.

Hisa za kampuni kubwa ya magari ya Japan, Toyota zilishuka kwa zaidi ya asilimia 2 na hisa za Nippon Steel pia zilishuka kwa zaidi ya asilimia 4.

Toyota imesema uamuzi wa Marekani " ungeathiri sana watengeneza magari na wanunuzi"
Trump amesema nini?
Trump ameahidi kuijenga tena sekta ya chuma na aluminiam nchini humo ambayo amesema imetendewa vibaya na nchi nyingine hasa China kwa miongo mingi.

“Kama nchi yako haiwezi kutengeza aluminiam na chuma ni kama hauna nchi tena,” amesema

"Tunahitaji watengenezaji wazuri wa aluminiam ili kujilinda"
Tangu aingie madarakani amekuwa akisema kuwa uingizaji wa bidhaa kutoka China umedhoofisha viwanda.

No comments:

Post a Comment