Saturday, 17 March 2018

Vigogo wakutana kutafuta mbinu za kumaliza mgogoro wa ardhi Kia


Vig

Vigogo waliokutana kujadili mgogoro wa ardhi Kia wakiangalia ramani ya wanavijiji.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo amekutana na mawaziri wa Ujenzi na Ardhi kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na mwendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), Kampuni ya Kadco.

Jafo amekutana jana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula kujadili mustakabali wa mgogoro huo uliodumu karibu miongo mwili.

Mgogoro huo unahusisha zaidi ya kaya 1,200 zilizopo katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha zinazotakiwa kupisha upanuzi wa uwanja huo.

Kaya hizo zipo katika vijiji vilivyopimwa kisheria lakini maeneo ya vijiji hivyo yanaingiliana na eneo la uwanja  wa Kia na hivyo kusabisha mgogoro baina ya menejimentinti ya uwanja huo na wananchi hao.

Hali hiyo ilipelekea kuundwa timu ya ufuatiliaji na utafutaji wa suluhu ya mgogoro huo ambayo inaundwa na wizara tatu za Tamisemi, Ujenzi na ya Ardhi wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali za ardhi na mawasiliano ya anga.

Kikao hicho kilimalizika kwa kuazimia kuwa vijiji hivyo vifanyiwe uthamini upya ili wananchi wa maeneo hayo walipwe fidia ili kuacha maeneo hayo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja cha ndege.

Kwa pamoja viongozi hao wamekubaliana kuanza mchakato wa kufuta hati za vijiji hivyo na kuanza mchakato wa kuwaelimisha wananchi kuhusu  umuhimu wa eneo hilo kwa maslahi mapana ya taifa.

Mgogoro kati ya wananchi wanaozunguka uwanja wa ndege wa Kia na kampuni ya Kadco umekuwepo tangu mwaka 1998.

No comments:

Post a Comment