Monday, 19 March 2018

Vijiji 50 vya Kishapu kunufaika na umeme wa Rea


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (aliyesimama mbele) akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea miradi ya umeme.
Mwandishi Wetu, Kishapu

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema serikali itaendelea  kusambaza nishati ya umeme katika vijiji vyote 50 vya wilaya ya Kishapu kama ambavyo iliahidi.

Amesema hayo wilayani hapa wakati  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipofanya ziara ya kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Kamati hiyo ikiwa kwenye vijiji vya Negezi na Bulimba ikiambatana pia na uongozi wa mkoa na wilaya, Mgalu amesema mpango wa usambazaji umeme ni wa awamu na kuwa wananchi wasiwe na hofu kwa kuwa kijiji kitafikiwa na mradi huo.

Ameongeza kuwa vijiji 33 kati ya 50 vitapata umeme wa Rea awamu hii ya tatu wakati 17 vitapata nishati hiyo kupitia njia kuu inayounganisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Tabora.

Kwa upande wake, kamati hiyo ya Bunge imesema wataendelea kuikumbusha Serikali iendelee kutimiza ahadi zake za kukamilisha miradi ya umeme kwa wananchi.

Iliwataka wananchi ambao wamepitiwa na miradi hiyo katika vijiji vyao kuichangamkia fursa na kuomba kuunganishiwa ili kupata nishati hiyo inayochochea maendeleo.

Aidha,  imewataka wananchi kuboresha aina za makazi yao kadiri ya uwezo wao kwa kujenga nyumba bora walizoezeka bati na kuachana na zile za tembe.

Katika ziara hiyo kijiji cha Bulimba kilichopo kwenye kata ya Ukenyenge kumezinduliwa huduma ya umeme mradi uliokamilshwa kupitia Rea na hivyo kutarajiwa kuwanufaisha wananchi wake.


No comments:

Post a Comment