Monday, 5 March 2018

Vipimo kubaini Nabii Tito mgonjwa wa akili vyasubiriwa mahakamani


Mary Meshack, Dodoma

MAHAKAMA ya wilaya ya Dodoma imeahirisha kesi ya Tito Machibya maarufu kama Nabii Tito baada ya vipimo vya kuthibitisha kwamba ana matatizo ya akili kutoka taasisi ya magonjwa ya akili ya Mirembe kutokamilika.

Akihirisha kesi hiyo, hakimu wa mahakama hiyo, Mwajuma Shelukindo amesema itatajwa tena Machi 19, mwaka huu.

Machibya anayetuhumiwa kwa kosa  la kutaka kujiua kwa kujikata na wembe na kujijeruhi kwenye maeneo ya tumbo Januari 25, mwaka huu, katika mtaa  wa Ng’ong’ona alitakiwa kufikishwa mahakamani leo na vielelezo kutoka taasisi ya Mirembe vinavyothibitisha iwapo ana magonjwa ya akili, lakini hakufika kutokana na vipimo hivyo kutowasilishwa kutoka Taasisi ya Mirembe.

Agizo la Tito kupimwa tena katika taasisi ya Mirembe ilitolewa Februari 5, mwaka huu, ambapo kesi hiyo ilitajwa ambapo ilidaiwa na hakimu wa mahakama hiyo kuwa vipimo bado havijakamilika na kufikia uamauzi wa kuahirisha kesi hiyo tena.
Mahakama ilitoa amri Tito apelekwe kupimwa katika taasisi ya Mirembe Isanga kwa mujibu wa kifungu namba 219 (2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Kifungu hicho kinasema, kama mshtakiwa atabainika kuwa kweli ana matatizo ya afya ya akili, mahakama itamwachia huru.


No comments:

Post a Comment