Thursday, 8 March 2018

Waafrika 10 walio tajiri zaidi duniani


Aliko Dangote

BWANYENYE kutoka Nigeria, Aliko Dangote ndiye mtu mweusi aliye tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa jarida la Forbes.

Kati ya watu 2,043 ambao wameorodheshwa kuwa mabilionea duniani katika orodha ya Forbes ya mwaka huu, ni watu 10 pekee ambao ni weusi.

Dangote amehifadhi taji la kuwa mtu mweusi tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa takriban dola za Marekani bilioni 14.1.

Anafuatiwa na Mnigeria mwenzake Mike Adenuga ambaye utajiri wake unakadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 5.3

Tajiri anayejihusisha na ujenzi ambaye ana uraia wa Saudi Arabia na Ethiopia Mohammed Al-Amoudi ambaye alikuwa na utajiri wa dola bilioni 8.4 aliondolewa kwenye orodha hiyo mwaka huu baada ya Forbes kuamua kuwaondoa mabilionea kutoka Saudi Arabia kwenye orodha hiyo.

Raia wa Zimbabwe aliyewekeza katika sekta ya mawasiliano, na ambaye hutoa fedha nyingi kwa hisani, Strive Masiyiwa, amejiunga na orodha ya watu weusi walio mabilionea. Ndiye mtu wa kwanza kutoka Zimbabwe kuwa bilionea.

Binti wa aliyekuwa rais wa Angola, Isabel dos Santos, Mmarekani anayejihusisha na vyombo vya habari Oprah Winfrey na tajiri wa mafuta kutoka Nigeria Folorunsho Alakija bado ndio wanawake pekee weusi kwenye orodha ya mabilionea duniani, kwa mujibu wa jarida hilo.

Marekani ndiyo nchi iliyo na mabilionea wengi duniani, ambapo ina mabilionea 585, ikifuatwa na China. Jimbo la California pekee lina mabilionea 144, zaidi kushinda mataifa yote isipokuwa Marekani na China.

Ujerumani ndiyo nchi inayoongoza Ulaya ikiwa na mabilionea 123. India ina mabilionea 119 nayo Urusi mabilionea 102. Kuna mabilionea 53 kutoka Uingereza kwa mujibu wa Forbes na idadi hiyo imeshuka kutoka 54 mwaka 2017.

No comments:

Post a Comment