Thursday, 15 March 2018

Wadau tiba asili, mbadala waomba serikali kuangalia utendaji kazi wa baraza lao

Claudia Kayombo

SIKU mbili baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile kuliagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuongeza kasi ya usajili wa dawa asili na mbadala, wadau wa tiba hiyo wanasema dhamira hiyo njema ya serikali haitafanikiwa kwa kuwa baraza hilo ni kikwazo.

Wakizungumza na glob hii kwa nyakati tofauti wamesema iwapo serikali imedhamiria kufanya hivyo, ikutane kwanza na waganga ambao ndiyo wadau wakubwa kupata maoni yao kabla ya kuliachia baraza hilo kusimamia kazi hiyo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Virutubisho ya Mandai, Mtaalam Abdallah Mandai amesema bila shaka serikali imetoa kauli hii ikiwa na dhamira njema lakini haijui iwapo baraza hilo halina nia njema na waganga wa tiba asili hapa nchini.

“Kwanza mtaalamu yeyote wa tiba asili au mbadala akienda katika ofisi za baraza hilo anapokelewa kwa dharau kama mchawi au jambazi, kama ni hivyo jitihada hizi zitafanikiwaje wakati baraza halina ushirikiano nao?,” alihoji.

Amefafanua kuwa ana amini serikali inapenda dawa za waganga walioko nchini zisajiliwe ndiyo maana imetoa gizo hilo, lakini haijui utata uliopo ndani ya baraza hivyo ni vema ikachunguza ukweli wa madai haya na kuufanyia kazi.

Amebainisha kuwa baraza hilo iwapo lingekuwa na nia thabiti ya kuzipa kipaumbele kazi za waganga lingewaita pale wanapokosea kuwakosoa ili waboreshe huduma zao zilingane na kiwango ambacho inataka badala yake wanawafungia kutoa huduma hizo.

Kuhusu kauli ya Naibu Waziri Dk. Ndugulile ya kulitaka baraza hilo kuongeza kasi ya kusimamia usajili huo, amesema kimsingi inaonesha dhamira njema ya serikali ya kuona matabibu walioko nchini wananufaika na ujuzi wao.

Pia amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya huku akibainisha kuwa kauli ya naibu waziri huyo ni msukumo kutoka juu.

Aliyekuwa mmiliki wa Kituo cha Tiba Asili cha Fore Plan, Dk. Juma Mwaka amesema baraza hilo ni kikwazo kwa kazi za tiba asili na mbadala hivyo serikali iliangalie upya kwani lingekuwa makini, tangu liundwe lisingesajili dawa tano pekee.

Amesema Tanzania inao waganga wa tiba asili na mbadala zaidi ya 60,000 kwanini iwe katika kipindi hicho ni dawa tano tu huku mmoja mwenye dawa nne ana asili ya Asia na mwingine ameolewa mzungu.

Mwaka amefafanua kuwa iwapo wizara ina nia ya dhati ya kusajili dawa asili na mbadala iwaite waganga ikae nao baada ya hapo itajua nini cha kufanya vinginevyo agizo hilo halitakuwa na maana kwa serikali na taifa.

Kuhusu uongozi wa baraza hilo, ameishauri serikali ione uwekano wa baraza kuongozwa na waganga wenyewe wa tiba hiyo badala ya wale walioko sasa ambapo miongoni mwao wamo wataalamu wa afya ya kinywa na meno huku wakiwa hawajui chochote kuhusu tiba hiyo.

 “Ukweli matabibu wa tiba asili nchini hatuwezi kufika mbali hata kidogo kwa kuwa wafanyakazi wa baraza wamekuwa kikwazo, mimi waliwahi kuniambia kwanini usifanye kazi nyingine, kwanini nisifanye hii ili kama kuna sehemu nakosea wanikosoe niboreshe kazi yangu, kauli zao ni za kuvunja moyo,” amesema Mwaka.

Kwa upande wake tatibu Maneno Tamba maarufu kama Dk Tamba amesema serikali inapaswa kujiuliza kwanini iwe ni dawa tano tu zilizosajiliwa, ifuatilie baraza itagundua kasoro nyingi.

Amesema utendaji kazi wa baraza hilo haulengi kuleta maboresha ya tiba asili nchini badala yake unataka kuirudisha katika tunguli na manyanga.

Amefafanua kuwa Rais Magufuli amesema Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati wa viwanda ikiwa ni pamoja na viwanda vya dawa asili na mbadala, lakini hali ilivyo ndani ya baraza hilo tiba asili  ibaki nyuma.

Naye Hassan Ibrahim  maarufu kama Dk. Manyuki amesema mazingira ya baraza yaliyo sasa hayawezi kuwasaidia waganga hivyo serikali iliunde upya baraza hilo.

Amesema matabibu wengi nchini hawana uwezo mzuri kifedha hivyo kabla ya kuendesha hamasa hiyo serikali ikae nao kuona itakavyoweza kuwasaidia hata wale wenye uwezo mdogo.

“Bila kukaa na wadau yaani waganga wenyewe wa tiba asili sisi waafrika hatuwezi kufika mbali, wageni ndiyo watakaopewa fursa ya kusajili dawa zao,” amesema Dk.Manyanyau.

No comments:

Post a Comment