Peter Simon
JESHI la Magereza limetiliana
saini na Asasi ya Technoserve kuendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa
wafungwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 30 waliopo magerezani
kwenye mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Katavi na Rukwa.
Hafla ya kutiliana saini makubaliano
hayo imefanyika katika ofisi za makao makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam ambapo
Technoserve iliwakilishwa na ofisa wake, Monsiapile Kajimbwa.
Akizungumza baada ya kutiliana
saini makubaliano hayo, Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk. Juma Malewa amesema mafunzo
hayo yatawapa uwezo wa kubaini na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi wafungwa hao ikiwemo kubuni na kuandaa mipango
ya biashara.
“Mafunzo haya yatawanufaisha sana
wafungwa waliopo magerezani katika mikoa hiyo kwani yatawajengea uwezo wa
kujitambua pamoja na kujipatia vipato halali badala ya kutenda uhalifu katika
jamii,” amesema Jenerali Malewa.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo
yatafanyika katika Chuo cha Ufundi cha Magereza Ruanda kilichopo mkoa wa Mbeya
ambapo wafungwa watajifunza nadharia na vitendo katika dhana nzima ya
ujasiriamali ikiwemo stadi za utengenezaji sabuni, ushonaji, useremala, ufumaji
sanjari na uandaaji wa mipango ya kibiashara.
Meneja Mkazi wa Technoserve, Monsiapile
Kajimbwa amesema hatua ya kutiliana saini makubalino hayo ni kuimarisha
ushirikiano kati ya asasi yake na Jeshi la Magereza katika kutoa mafunzo kwa
wafungwa ili waweze kupata ujuzi kupitia program hiyo.
No comments:
Post a Comment