WAFUNGWA watatu walisomea gerezani wamehitimu shahada katika sheria,
ikiwa ni mara ya kwanza kwa wafungwa nchini Uganda kufuzu shahada hiyo.
Mpango huo
unaofanikishwa na Mradi wa wafungwa barani Afrika kwa ushirikiano na chuo kikuu
cha London, unanuia kuwapa wafungwa fursa ya kushiriki kikamilifu katika
taratibu za kutafuta haki.
Kuhitimu kwa
watatu hao kutoka Gereza Kuu la Luzira kumetazamwa kama ishara ya mwamko mpya
katika mfumo wa marekebisho magerezani nchini Uganda.
Pascal Kakuru,
Suzzan Kigula na Moses Ekwam walipokea shahada za digree huku wakiwa wamevalia
sare nyeusi za kuhitimu.
Moses Ekwam
mmoja wa waliohitimu alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano lakini
alihudumu miaka minne baada ya kukutwa hana hatia.
Kwa miaka hiyo
minne alipokuwa gerezani alianza kusomea somo la sheria. Ekwam kwa hivi sasa ni
mwendesha mashtaka wa jeshi la Uganda.
“Mimi nilikuja hapa
nikaona kukaa kuangalia mpira tu niliona shule iko ndani kwa hivyo nikaamua
kujiunga na shule A level nikapita vizuri 210 hadi sasa hivi niko wakili,” ameiambia
BBC.
Mwenzake Pascal
alikuwa akitumikia kifungo kwa makosa ya uhaini na hivi sasa anaelekea kumaliza
kifungo chake baada ya kupata msamaha. Anaeleza anavyolenga kutumia utaalamu
wake katika sheria
“Ninao mpango
wa kuzungumzia wale watu wanaoteseka wale watoto, kinamama, wafungwa wakimbizi
ni watu hodari sana huwezi kuwaongelea wawe kama wanaharakati watu kama hao.
“Kutakuwa na
ulimwengu vitu kadhaa vya watu kama hao kwa hivyo nina mpango wa kuwazungumzia
mahali popote wapo si kwa nchi ya Uganda peke yake bali ulimwengu mzima popote
nitakapopata nafasi ya kuwasaidia watu kama hao.
Katika ripoti
ya hivi karibuni Jarida la Afrika la masuala ya uhalifu na haki, idara ya
magereza nchini Uganda imewekwa katika nafasi ya kwanza barani Afrika kwenye
suala la mageuzi. Hata hivyo, bado kuna changamoto katika kuzingatia haki za
wafungwa.
Owinyi Dollo ni
naibu jaji mkuu nchini Uganda: "Unaanza kujiuliza kweli kama hukumu ya
kifo inapaswa kuwa katika sheria zetu, unahoji kwa sababu mtu ambaye alivunja
sheria jana anaweza kubadirika na kuwa mtu mwenye ushawishi mwema leo.
Kwa kuhitimu
wafungwa hao watatu wanafuata nyayo za rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson
Mandela aliyejiimarisha kitaaluma wakati akiwa gerezani jambo linalowapa
matumaini wafungwa wengi na pia kuongeza msukumo wa mageuzi zaidi magerezani.
Nchini Kenya,
wafungwa wamewahi kusomea sheria na kuhitimu na baadhi hata kuwasaidia wenzao
kupata uhuru. Peter Ouko, mmoja wao, kwa sasa ni balozi wa shirika la Africa
Prisons Project.
Amekuwa
amehukumiwa kifo na kuwa mfungwa kwa miaka kumi na minane kabla ya kupunguziwa
kifungo na kuwa kifungo cha maisha na kisha kuachiliwa huru kwa msamaha wa
rais. Alikuwa amepatikana na kosa la kumuua mkewe.
No comments:
Post a Comment