Tuesday, 13 March 2018

Walimu sekondari wapatiwa mafunzo ya Tehama


Mhandisi Atashasta Nditiye 

Mwandishi Wetu, Dodoma

WALIMU 327 kutoka shule 109 za sekondari nchini wanapatiwa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ili kuwawezesha kutumia teknolijia hiyo kufundishia.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amefungua mafunzo hayo mkoani hapa kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa. Mafunzo hayo ya siku tano, yanafanyika kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mhandisi Nditiye amefafanua kuwa Serikali imeona ombwe lililoko baina ya shule za umma na zile binafsi katika masuala yanayohusu Tehama, hivyo imekasimu jukumu hilo kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili kulitafutia ufumbuzi ambapo pamoja na mambo mengine shule zote za umma zitaunganishwa na mtandao wa intaneti na kupatiwa vifaa vya Tehama.

Mhandisi Nditiye amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuboresha sekta ya elimu nchini kwa kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapatiwa miundombinu inayohitajika ambayo ni pamoja na  vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuboresha maslahi ya walimu.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, Justina Mashiba amesema mfuko umeandaa mafunzo ambayo yatatolewa kwa walimu kwenye vituo viwili ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa UCSAF itatoa kompyuta 545 kwa shule 109 ambapo kila moja itapata tano. Amesema mafunzo hayo ni ya awamu ya pili baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza yaliyofanyika mwaka jana ambapo walimu 286 walipatiwa mafunzo kama hayo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Aloyce Mvuma amemhakikishia Mhandisi Nditiye kuwa Chuo kina wakufunzi wenye weledi kwa ngazi ya kimataifa.

Mwakilishi wa walimu, Sammy Sanga kutoka wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka na kuwapatia mafunzo hayo ambapo yatawawezesha kwenda kufundishia walimu wenzao na wanafunzi ili kuiwezesha Serikali kufikia azma  yake ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa sekondari za umma nchini.

No comments:

Post a Comment