Saturday, 17 March 2018

Wanafunzi waaswa kuwa makini na mitandaoThadayo Ringo

Mary Meshack, Dodoma

NAIBU Mkurugenzi Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Thadayo Ringo, amewaasa wanafunzi kuwa makini wanapotumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii kwa ujumla.

 Akizungumza na wanafunzi wa  shule ya sekondari ya wasichana Msalato iliyopo Manispaa ya Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Haki za Mtumiaji  Duniani, Mkurugenzi huyo amesema, katika mitandao wapo waongo na wezi iwapo wakiwafuata wanaweza kuwaharibia matarajio ya maisha yao.

Amewataka kutumia vifaa vyote vya mawasiliano kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla na si kwenye mambo yasiyokuwa na tija.

“Wanawake wana tabia ya kuwaamini watu na wengi wao ni waongo, usimwamini mtu yeyote kwenye mitandao maana waongo ni wengi,”amesema.

Pia amewataka wanafunzi hao kuacha kuangalia picha za ngono na tamthilia zinazohusu maisha na mahusiano maana vyote kwa pamoja havina faida  yoyote kwao zaidi ya kuwapotezea muda wao wa kujisomea.

Kwa upande wake ofisa Mwandamizi Masafa wa mjini hapa, Boniface Ngeela akizungumzia kuhusu wajibu wa mteja amesema kila mmoja anapaswa kutumia mitandao kwa kuzingatia sheria za nchi.

Vile vile amesema,kila mteja anapaswa kuhifadhi mazingira na kutunza nyenzo za mawasiliano ikiwemo miundombinu ya mawasiliano.

No comments:

Post a Comment