Friday, 2 March 2018

Wanamgambo wa al-Shabab waua polisi watanoWanamgambo wa Kiislamu wa la al-Shabab
WANAMGAMBO wa Kiislamu wa al-Shabaab katika eneo la Fino, Kaunti ya Mandera, kaskazini mwa Kenya, wamewaua askari polisi watano na wengine watatu kujeruhiwa.
Naibu kamishna mkuu wa eneo hilo, Eric Oronyi anakisia kuwa kati ya wapiganaji 70 au 100 hivi waliokuwa na silaha kali, walivamia kambi ya polisi mapema leo alfajiri na kuiteketeza kabisa.
Amesema maofisa wengine watatu walijeruhiwa, na mmoja wao yuko katika hali mbaya, shirika la habari la Reuters limesema.
Oronyi amesema washambuliaji hao waliharibu mtambo wa mawasiliano, kabla ya kuvamia kambi hiyo.
“Mnara wa mawasiliano, ambao ulikuwa ukilindwa na polisi wa akiba, ulipigwa bomu na kwa sasa, hakuna mawasiliano yoyote ya simu hata ya rununu katika eneo hilo”, amesema Oronyi.
Kundi hilo la wapiganaji, ambalo limekuwa likitekeleza mashambulio mara kwa mara kutokea nchi jirani ya Somalia, limekuwa likiwalenga maofisa wa usalama na magari ya umma, kuvamia maskani ya watu na machimbo ya mawe na kuwaua watu wengi kwa kuwapiga risasi.
Kaunti ya Mandera, inapakana na nchi ya Somalia, jambo ambalo limewaacha wapiganaji hao kutekeleza maovu yao kwa urahisi.
Katika mwaka mmoja uliopita, kundi hilo la wapiganaji wa Kiislamu, limekiri kutekeleza mauaji ya watu kadha eneo la Mandera.


No comments:

Post a Comment