Wednesday, 21 March 2018

Wanawake kupewa kipaumbele miradi ya ujenzi
Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema Myeya,  akifafanua jambo kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake (hawapo pichani), mkoani Morogoro, wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kuhusu njia mbadala za kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa wingi katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara.

Mwandishi Wetu, Morogoro

UWIANO wa wanawake katika miradi mingi ya ujenzi nchini ikiwemo matengenezo na usimamizi wa barabara unaelezwa kufikia asilimia 6 na 7 kati ya wahandisi 100 ukilinganisha na wanaume katika Sekta ya hiyo.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, ametoa kauli hiyo wakati akifungua semina elekezi kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara nchini na kufafanua kuwa hali hiyo inatokana na ushirikishwaji mdogo wa wanawake katika kazi hizo.

 Aidha, Mhandisi Kiula,  amesisitiza umuhimu wa semina hiyo kwa waratibu hao ili kuwajengea uwezo, ujuzi na njia mbadala za kuongeza idadi ya wanawake watakaoshiriki kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara pia  kuhamasisha wanawake wengine kushiriki kazi hizo.

“Serikali sasa inalenga kuwawezesha makadarasi wanawake kufikia madaraja ya juu ya ukandarasi ili kuweza kuinua kipato chao na kuondokana na umaskini katika familia na jamii kwa ujumla,” amesisitiza Mhandisi Kiula.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo elekezi yatawasaidia kupambanua masuala muhimu yatakayoweza kurahisisha uratibu na usimamizi mzuri katika utendaji kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kwa ufanisi zaidi.

"Ni maratajio yangu mkimaliza mafunzo haya mtatekeleza kazi zenu kwa ufanisi zaidi na kuleta matokeo chanya kwa jamii na taifa,”  amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji  Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema Myeya, amesema kazi kuu za waratibu hao ni kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa wingi katika kazi za barabara katika mikoa yote ili kupanua wigo wa maendeleo katika jamii na mafanikio katika kazi hizo.

Mhandisi Myeya, ametaja mada zitakazojadiliwa katika semina hiyo kuwa ni masuala ya jinsia na namna ambavyo Serikali inayashughulikia ikiwemo sheria ya ujenzi na namna inavyosisitiza ushiriki wa wanawake na kuipitia sheria ya manunuzi na kuona maeneo ambayo yanatoa kipaumbele kwa wanawake.

Mada nyingine ni kuangalia mchakato wa usajili kwa kampuni ya wanawake, kupitia mwongozo wa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika kazi za barabara na masuala mtambuka, namna ya kuandaa zabuni ambazo zinaakisi mahitaji ya wanawake na ufanisi wa teknolojia ya nguvu kazi katika kufanya matengenezo ya barabara.

Ushirikishwaji wanawake katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kitaifa ulianza mwaka 1992 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Shinyanga, Mwanza na Mtwara, hii ni kutokana na kazi hizo kufanywa na wanaume hasa kwenye nyanja za makandarasi na wahandisi washauri.

No comments:

Post a Comment