Tuesday, 27 March 2018

Wataalam wamhakikishia Makonda kutoa msaada kwa kinamama bila upendeleo


Paul Makonda 

JOPO la wataalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa serikali, maofisa ustawi wa jamii, wanasheria pamoja na Askari Polisi kutoka Dawati la Jinsia  wamemuhakikishia mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa wamejidhatiti vema kuwasikiliza kinamama waliotelekezwa na hawapatiwi fedha za matunzo ya mtoto kwenye mchakato wa siku tano za kuwapatia msaada wa kisheria kinamama hao linalotaraji kuanza April 09, mwaka huu. 

Akizungumza na wataalamu hao, RC Makonda amesema tatizo la kinamama waliotelekezwa ni kubwa na limekuwa likisababisha wengi wao na watoto kuishi maisha ya taabu na kusababisha ongezeko la watoto wa mitaani na vizazi vya watoto wenye chuki na baba zao.

RC Makonda amesema lengo la kufanya hivyo sio ugomvi bali ni kumwezesha mtoto kupata mahitaji ili aweze kuitumia vema fursa ya elimu bure chini ya serikali ya Awamu ya Tano. 

Aidha, RC Makonda amewahimiza wataalamu hao kuhakikisha wanawasikiliza kinamama kwa umakini na kusimamia haki bila upendeleo.

Pamoja na hayo RC Makonda amesema wapo kinababa ambao wameanza kutoa fedha ya matunzo ya mtoto baada ya kusikia tangazo ambapo amewasihi kinamama hao kufika April 09 kwa ajili ya kuonana na wataalamu ili waweke makubaliano kwenye mfumo rasmi wa maandishi.

No comments:

Post a Comment