Monday, 19 March 2018

Watakiwa kuvipa kisogo vitendo vya rushwa kutoka kwa wananchi


Ummy Mwalimu 

WATUMISHI wa sekta ya afya wametakiwa kujiepusha na vitendo vya kutaka rushwa kutoka kwa wananchi wanapokuwa sehemu zao za kazi ili kuendana na maadili ya utumishi wa umma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo katika kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jana Dar es Salaam kujadili mustakabari wa utoaji wa huduma za afya.

“Marufuku watumishi wa sekta ya afya nchini kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na kama wapo naomba waache mara moja kwani atakayebainika anajihusisha na rushwa, sheria itafuata mkondo wake mara moja” amesema Waziri Ummy.

Aidha, amesema watumishi wa sekta ya afya hasa katika sehemu ya kutolea huduma za afya wanatakiwa kuwa na lugha nzuri kwa wananchi pindi wanapotoa huduma sehemu zao za kazi.

Mbali na hayo Waziri Ummy amewataka watumishi wa sekta ya afya kutoa elimu kuhusu magonjwa yasioambukiza kwa jamii kwa kuwa yamekuwa yakiongezeka kila kukicha kwa vile tu haina uelewa nayo wa kutosha.

“Watumishi wa afya wanatakiwa kuwa mfano hasa katika kufanya mazoezi, kula lishe bora pamoja na kutoa elimu ya magonjwa mbalimbali ili kuisaidia kuondoa ongezeko la magonjwa yasioambukiza” amesema Waziri Ummy.

Aidha, amesema ili kufikia adhma ya Rais Dk. Jonh Magufuli ya kujenga uchumi wa viwanda ni lazima kuzingatia utoaji wa huduma bora za afya ili kuwa na wananchi wenye afya ambao watasukuma gurudumu kufikia lengo hilo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Balaza la Wafanya kazi TUGHE, Nsubisi Mwasandende amesema katika kutatua changamoto za magonjwa mbalimbali watendaji wa Wizara ya Afya wanatakiwa kuzingatia hali ya upatikanaji wa chanjo ili kuboresha huduma za afya.

Aidha,  Mwasandende amesema watumishi wanatakiwa kulifanyia kazi haraka agizo la Waziri Ummy Mwalimu la kutokomeza vitendo vya rushwa ambalo ni moja la azimio la katiba ya baraza la wafanyakazi.

No comments:

Post a Comment