Saturday, 10 March 2018

‘Watanzania hatukutakiwa tuwe ombaomba’


Rais Dk. John Magufuli

Mwandishi Wetu, Geita

RAIS Dk. John Magufuli amesema watanzania hawakutakiwa kuwa maskini kwani nchi ina maliasili nyingi ikiwemo madini ya dhahabu lakini wajanja wamelifikisha taifa lilipo sasa.

Amesema Tanzania inaweza kuwa taifa linalojitegemea ndiyo maana katika Awamu hii nchi ipo miongoni mwa mataifa matano katika Afrika ambayo uchumi wake unapanda kwa kasi kubwa.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua barabara ya Uyovu Bwanga, Bukombe, mkoani Geita yenye urefu wa kilomita 40.

Hata hivyo, amesema hali ya uchumi ina imarika kutokana na amani iliyo nchini hivyo taifa lisifikie hatua ambayo mataifa ya Ruanda na Burundi yaliingia katika machafuko mwaka 1994 ambapo watu wengi wakiwemo watoto wadogo walipoteza maisha yao.

Amesema amani ambayo iliasisiwa na Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, imeendelea kulindwa na waliomfuata naye ameahidi kuendelea kuilinda kwa nguvu zake zote.

Amewataka wazee wa mila, viongozi wa dini na akina mama ambao wana jukumu kubwa la kulea familia wahakikishe wanawaeleza vijana na watoto kuhusu umuhimu wa kulinda amani.

Amesema serikali yake lazima iwabebe wanyonge ambao wameteseka kutokana na changamoto mbalimbali za maisha kwa muda mrefu hapa nchini.

“Nina fahamu mnahitaji maeneo ya kulima na kuchungia mifugo na wengine mnataka hata kuingiza mifugo yenu  katika hifadhi, subirini kwanza hili tulifanyie kazi,” amesema.

Amesema umefika wakati serikali ijipange kuangalia namna ya kutoa baadhi ya mapori ya hifadhi kwa ajili ya wananchi kwani yalitengwa baada ya uhuru mwaka 1961 ambapo idadi ya watu ilikuwa milioni 10, sasa wapo karibu milioni 54 hivyo ni vema baadhi ya mapori yakatolewa kwa ajili ya wananchi.

Rais Dk. Mafufuli aliwashukuru wananchi wa Bukombe kwa kumchagua pamoja na mbunge Dotto Biteko kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Ameahidi kuendelea kuwa mtumishi wao mwema na mwadilifu.

Amewataka wananchi kutunza barabara zote zinazojengwa nchini pia amewataka madereva kuwa makini wanapoendesha magari huku akijua kuwa wameba roho za watu.

No comments:

Post a Comment