Saturday, 17 March 2018

Watumia jina la Rais Kikwete kujipatia fedha kwa udanganyifu


 Rais Jakaya Kikwete

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia wanawake watatu kwa kosa la kutumia jina la Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na familia yake kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es salaam, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema Februari 23 mwaka huu kuliripotiwa kuwepo watu wanaotumia jina la kiongozi huyo kushawishi wengine kupata mkopo wa fedha kwa kujitangaza kupitia ukurasa wa facebook uitwao, ‘Jakaya Kikwete Focus Vicoba’ na ‘Ridhiwan Kikwete Focus Vicoba’
Kamanda Mambosasa amewataja washukiwa hao kuwa ni Mase Uledi (41), mkazi wa Kitunda, Khadija Khamis (42), mkazi wa Tabata na Mwange Uled (33), mkazi wa mkoa wa Bukoba.
Washukiwa hao walikamatwa wakiwa na simu za mkononi 12 zenye laini za mitandao mbalimbali huku wakiwa na nyingine 10 zisizo kuwa ndani ya simu ambazo huzitumia ili kufanikisha uhalifu huo.
Washukiwa hao walifungua ukurasa huo wa facebook na wamekuwa wakitumia laini hizo za simu kuwapigia na kuwatumia ujumbe mfupi wananchi ili kuwashawishi kujiunga kwenye taasisi hizo na kufanyia miamala ya fedha kutoka kwa wakopaji wanaoshawishika.
Aidha, Kamanda Mambosasa amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili.
Lazaro Mambosasa

No comments:

Post a Comment