Saturday, 24 March 2018

Waziri Mkuu aridhishwa maendeleo ya ujenzi wa JNIAWaziri  Mkuu Kassim Majaliwa katikati  mwenye tai akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana (March 23/2018).

Kushoto kwa Waziri Mkuu ni Mkuu wa mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda na kulia ni msimamizi wa mradi huo Mhandisi Julius Ndyamukama.  


Peter Simon

WAZIRI Mkuu  Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na kusema ameridhishwa na maendeleo yake.

Mradi wa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Juni 2019 na utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa 24 kwa wakati mmoja, pamoja na kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka.

Waziri Mkuu ambaye ametembelea mradi huo jana (Ijumaa, Machi 23, 2018) amesema amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo pamoja na kukuta Watanzania wengi wakishiriki katika kazi za ujenzi.

“Serikali imejiimarisha katika kuboresha usafiri wa anga, ambapo kukamilika kwa jengo hili kutachangia ongezeko la ndege kubwa nyingi kutua nchini. Pia sekta ya utalii nayo itaimarika kwa kuwa watalii wanaoingia nchini wataongezeka,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya ujenzi wa jengo hilo, pia Serikali inaendelea kuvikarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwemo cha Musoma, Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea ili kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini. 


No comments:

Post a Comment