Tuesday, 20 March 2018

WB yaipongeza mahakama kwa kufanya maboresho


Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahimu Juma akizungumza na mgeni wake Nicola Smithers ambaye ni Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB).

Peter Simon

MENEJA wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Nicola Smithers ameipongeza mahakama kwa kutekeleza mradi wa maboresho wa huduma za kimahakama.

Smithers ametoa pongezi hizo jana Machi 19, alipokutana na Jaji mkuu  Prof. Ibrahim Juma ofisini kwake Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam ambapo alipata nafasi ya kuzungumza naye pamoja na viongozi wengine wa mahakama akiwemo Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

 “Nimefurahishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maboresho ya huduma za mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, hususan katika eneo la uondoaji mlundikano wa mashauri,” amesema Smithers.

Akimkaribisha ofisini kwake, Jaji Prof. Juma amemueleza Smithers kuhusu maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ndani ya mahakama hapa nchini yote yakiwalenga wananchi ambao ndio wateja wa mahakama hizo.

“Miongoni mwa maeneo ambayo tunayoendelea kupambana nayo ili kurejesha imani ya wananchi kwa mahakama ni pamoja na rushwa, katika hili tumefanya jitihada kadhaa ikiwa ni pamoja na kusambaza mabango yenye ujumbe wa kupinga rushwa na kuyasambaza katika ofisi za mahakama kote nchini pamoja na kusambaza simu za kuwawezesha wananchi wenye malalamiko kutuma jumbe zao ili yaweze kufanyiwa kazi,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu amezungumzia kuhusu uamuzi wa utoaji wa nakala za hukumu bure kwa wananchi wenye kesi ili kuwarahisishia wenye kipato cha chini kupata haki zao pia.

Akizungumzia huduma katika mahakama za mwanzo wananchi wengi wanahitaji huduma hizo hivyo kuna haja ya kusogeza karibu nao zaidi.

“Mfano hivi karibuni nilifanya ziara mkoani Tabora, miongoni mwa maeneo ambayo yapo mbali kufikika kutokana na jiografia yake, maeneo kama haya yanatakiwa kuwa na huduma ya mahakama inayotembea ‘Mobile Court’,” amesema.

Smithers alikuwa nchini akitokea Washington D.C zilipo ofisi cha Benki ya Dunia na kwamba amefanya ziara yake  kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maboresho ya huduma za mahakama ambao unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya mahakama ya Tanzania na WB.

Maeneo muhimu yanaotekelezwa na mradi huo ni pamoja na mapambano dhidi ya rushwa, ambapo inaangazia ni kwa jinsi gani mahakama pamoja na wadau wengine wanaweza kushirikiana katika kupiga vita vitendo vya rushwa.

Maeneo mengine ni ushirikishaji wadau katika masuala yote ya utoaji haki na kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.

No comments:

Post a Comment