Wednesday, 25 April 2018

Bobali aomba fedha za barabara ziongezwe Lindi


Hamidu Bobali 

Suleiman Kasei, Dodoma

MBUNGE wa Mchinga, mkoani Lindi, Hamidu Bobali (CUF), ameiomba Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuongeza fedha za ujenzi wa barabara katika mkoa huo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19.

Bobali ameyasema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati akichangia kwenye mjadala wa bajati ya wizara hiyo iliyowasilishwa Aprili 23 na Waziri Profesa Makame Mbarawa.

Amesema wizara hiyo imetengewa takribani theluthi moja ya bajeti yote ya nchi huku mkoa wa Lindi ukitengewa sh. mil  800 kwa ajili ya utengenezaji na ukarabati wa kilomita 629 fedha ambazo ni kidogo.

Mbunge huyo amesema asilimia kubwa ya miundombinu ya barabara katika mkoa huo imeharibika katika kipindi kifupi hali ambayo inaonesha kuwa ubora haukuzingatiwa wakati wa ujenzi na kwamba fedha zilizotengwa hazitoshi.

“Mkoa una barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 629 umetengewa sh. milioni 800 lakini mikoa yenye barabara zenye kilomita 400 zimetengewa fedha nyingi hii sio sawa naomba waziri aliangalie,” amesema.

Amesema kwa sasa mkoa huo umepata fursa nyingi za kiuchumi kama kilimo cha korosho, ufuta na mazao  hivyo upo umuhimu wa uwepo barabara zenye ubora zinazoweza kupitika mwaka mzima.

Bobali ameongeza kuwa kutokana na mvua ambazo zimenyesha hivi karibuni barabara ya Lindi hadi Dar es Salaam imejaa mashimo ambayo yanasababisha ajali na uharibifu wa magari ya mizigo.

Aidha, mbunge huyo ameomba serikali kupandisha hadhi barabara ya Chikonji, Nangalu hadi Milola yenye urefu zaidi ya kilomita 100 kutoka halmashauri, ili iweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Halikadhalika Bobali ameomba Serikali kuhakikisha kuwa mfumo mawasiliano kwa wote unatekelezwa katika vijiji vyote jimboni hapo.

“Katika bajeti nimepata vijiji viwili na vijiji zaidi ya 15 vikibakia naomba hili lifanyiwe kazi,” amesema.

Ametaja baadhi ya vijiji ambavyo havina mawasiliano ni Mputwa, Kiwawa, Namkongo, Mvuleni, Ruvu, Namwangala na Kijiweni.

Aidha, Bobali ameitaka wizara hiyo kuhakikisha kuwa viwanja vya ndege nchini vinawekewa taa ili vifanye kazi saa 24 tofauti na ilivyo sasa ambapo vinafanya kazi saa 12.

Amesema hakuna faida ambayo itapatikana kama ndege zinazonunuliwa kwa gharama kubwa na kufanya kazi mchana pekee kama vile hakuna amani.

Bobali amesema ni vema jitihada zikaongezwa katika kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo inakamilisha mchakato wa usafiri wa anga.

No comments:

Post a Comment