Monday, 23 April 2018

Daraja la Nyerere laliingizia taifa mabilioni


Daraja la Nyerere

Peter Simon

DARAJA la Nyerere, Kigamboni Dar es Salaam, limeingiza sh. bilioni 14.9 kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi mwaka huu (2018).

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa hivi karibuni kwenye mkutano mkuu wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), makusanyo hayo ni wastani wa sh. milioni 650 kwa mwezi. Makusanyo hayo yametokana na wastani wa magari 10,393 yanayopita kwa siku.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara amesema mafanikio hayo yametokana na uamuzi wa kusimamia uendeshaji wa daraja hilo kwa kutumia wafanyakazi wake.

“Kutokana na uwekezaji huo shirika linategemea kupata sh. bilioni 14.53 zitakapoiva. Kwa maana hiyo hadi sasa thamani ya makusanyo ni sawa na shilingi bilioni 29.4.

“Mtindo huu wa uendeshaji (kutumia wafanyakazi wa shirika) unatoa uhakika wa kuendesha daraja kwa faida pamoja na kurudisha fedha za wanachama,” amesema.

Daraja la Nyerere lenye urefu mita 680 lilizinduliwa Aprili 19, 2016 na Rais John Magufuli, ujenzi wake ulianza mwaka 2012 na kufanywa na kampuni ya China Railway 15 Group ikishirikiana na kampuni ya China Bridge Engineering Group ambapo ujenzi wake uligharamiwa na serikali kwa asilimia 40 na NSSF kwa asilimia 60.

No comments:

Post a Comment