Friday, 13 April 2018

DRC yasusia mkutano ulioandaliwa kuisaidia nchi hiyo


Rais wa DRC, Joseph Kabila.
UMOJA wa Mataifa leo unafanya mkutano maalum mjini Geneva Uswizi kuchangisha fedha za kukabiliana na janga la kibinaadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mashirika ya misaada yanasema zaidi ya watu milioni 5 wamelazimika kuyatoroka makazi yao kwasababu ya mapigano katika sehemu tofauti za nchi hiyo kubwa.
Lakini serikali ya DRC imekataa kuhudhuria mkutano huo wa ufadhili ikisema kwamba hali inafanywa kuwa mbaya wakati ni kinyume cha hicho.
Mkutano huo umedhamiriwa kuchangisha dola bilioni 1.7 kupunguza uzito wa inachotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni janga kubwa la binadamu nchini Congo.
Hadi sasa serikali ya DRC haijajibu mualiko wa Umoja wa Mataifa ikisema taasisi hiyo kuu imetilia chumvi hali halisi nchini na ukubwa wa tatizo lililopo.
Mashirika ya misaada yanasema watu milioni tano wamelazimika kuyatoroka makazi yao kutokana na ghasia, mapigano, njaa na ukosefu wa utulivu na kwamba maelfu ya raia wa Congo wamelazimika kutafuta hifadhi Magharibi mwa Uganda.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu ndani ya DRC wamezusha wasiwasi kutokana na hatua hiyo ya serikali kususia mkutano huo mkuu mjini Geneva.
Wasiwasi wa aina hiyo pia umetolewa na baadhi ya raia wanosema kwamba wataendelea kuteseka bila ya msaada wa kimataifa.
Mashirika ya misaada yanasema DRC inateseka katika janga kubwa lenye uzito la kibinaadamu lililosahaulika kwa muda mrefu.
Kuna watu milioni 13 wanaohitaji usaidizi: miongoni mwao watoto milioni 2 wanaugua utapiamlo mbaya, na watu milioni 4.5 wamepoteza makazi yao.
Lakini tathmini hii ya mashirika ya misaada imeiudhi serikali ya DRC. Inatizama kiwango cha daraja la tatu kilichowekwa cha hali ya janga hilo kuwa kama tusi.
Na ndio sababu ikachukua hatua hii ambayo haikutarajiwa ya kususia mkutano wa Geneva.
Hata hivyo maofisa wa Umoja wa Mataifa wanatumai kwamba wanadiplomasia wa Congo watabadili uamuzi wao na watahudhuria mkutano huo leo.
Ni wazi kwamba mkutano wenyewe utaendelea licha ya chochote kile kitachotokea, wanaharakati wanasema maisha ya mamilioni ya watu yamo hatarini.

No comments:

Post a Comment