Sunday, 29 April 2018

Embe tunda lililosheheni faida nyingi


Embe

MAKABILA mengi hapa nchini yanapanda miembe kwa ajili ya matunda. Matunda ya miembe yanayojulikana kama embe, ni maarufu sana hapa nchini.
Radha tamu ya embe bila shaka ndiyo inaongeza umaarufu wa tunda hilo na hivyo jamii kubwa zaidi kulistawisha zao hilo lenye majani yenye rangi ya kijani.

Matunda ya embe ambayo hutofautiana ukubwa, mengi huwa na rangi ya kijani, njano ama nyekundu.

Embe inaweza kuiva ikiwa mtini lakini ili kuzuia uharibifu kutoka kwa ndege, wakulima huamua huvuna mara tu inapokomaa kwa kuangusha ikiwa bado haijaiva.

Utagundua kuwa embe imekomaa kwa kuiangalia rangi kwani hubadilika kutoka rangi ya kijani hadi ya manjano au nyekundu.

Kuna aina nyingi za embe zinazostawishwa hapa nchini miongoni mwazo ni dodo, embe maji, embe bolibo,  embe nuka na embe sikio la punda.
Tunda hilo linaliwa kama lilivyo lakini pia linaweza kutengenezwa juisi ambayo mara nyingi inakuwa na virutubisho vingi vinavyopatikana katika tunda hilo.

Hata hivyo, mtaalamu wa tiba, lishe na virutubisho, Abdallah Mandai anasema mmea huo kwa ujumla una faida nyingi kuanzia mizizi, shina, majani na hata maua.

Anasema majani ya mwembe yanasaidia kwa wanaosumbuliwa na maradhi ya pumu na harufu mbaya ya mdomo. Pia yakitumiwa ipasavyo yana uwezo mkubwa wa kusaidia kwa wanaugua malaria sugu.

"Chukua majani ya mwembe yakaushe katika kivuli ili kutoiondoa alkolaidi iliyomo ndani ya majani hayo ambayo ni muhimu sana katika tiba.

"Unaweza kuwa mtu mtanashati kwa namna yoyote lakini kama una tatizo la kutoa harufu katika kinywa bado thamani yako itapungua, hivyo tumia majani ya mwembe ambayo ni suluhisho la tatizo hilo," anasema.

Anaongeza kuwa wanawake wengi wanaonyonyesha hukabiliwa kwa kiwango kikubwa na changamoto ya uhaba wa maziwa hivyo watumie maua ya mwembe kukabiliana na tatizo hilo.

Mtaalamu huyo anasema unga unaotokana na maua ya mwembe ukichanganywa na maji moto, au asali ama maziwa unasaidia kuondoa changamoto hiyo.

Kuhusu tunda la mwembe anasema linasaidia katika usanisi wa chakula tumboni kwa kuwa limesheheni vitamini A, C, D.

"Katika embe kuna kiwango kikubwa cha madini ya chuma na chumvi, tunda hili pia linaongeza hamu ya kula chakula kwa anayelitumia. Kokwa la embe lenyewe linasaidia kwa akina mama katika tatizo la uzazi.

"Linazibua mirija ya uzazi na linabalansi hedhi ya mwanamke hususan kwa yule ambaye anakwenda bila mpangilio.Twanga kokwa, unga wake tumia katika maji moto inazibua mirija ya uzazi inazua utokaji damu, inaondoa uvimbe katika tumbo la uzazi,"anasema.

Pia anasema gome la mwembe linasaidia katika tatizo la miguu kuwaka moto au kufa ganzi ambapo maradhi hayo yanasababishwa na moyo kuelemewa.

"Unapotumia unga wa magome uliochanganywa na mafuta kwa kupaka kwenye miguu unazuia maumivu au kuondoa kabisa ganzi," anatanabaisha.

Anasema unga wa gome pia ukichanganywa katika uji kikombe cha chai na kijiko cha chai, pia wanawake wenye matatizo ya maumivu wakati wa hedhi pia inasaidia sana kuondoa mauamivu.

Mizizi ya mwembe pia inasaidia kuondokana na maradhi kadhaa hivyo kuufanya mti huo kuwa uliosheheni tiba kwa binadamu.

No comments:

Post a Comment