Wednesday, 4 April 2018

Gavana atuhumiwa kwa ubakaji


NAIBU Gavana wa jimbo la Ikweta Kusini Magharibi mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC),Tathy Bikamba ameshtakiwa kwa tuhuma za ubakaji wa binti wa miaka 20 ambaye inadaiwa alimfanyia unyama huo baada ya kumpa dawa za kulevya.
Gavana huyo anatarajiwa kufikishwa Kinshasa kujibu tuhuma hizo mahakamani, ingawa wakili wake ametupilia mbali tuhuma hizo. Taarifa kutoka duru za karibu za uchunguzi wa kesi hiyo ya kubaka zinasema gavana huyo alimbaka binti huyo siku ya Jumamosi.
Bikamba ambaye kwa sasa yuko gerezani anatarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo ili aweze kujibu mashtaka yake ya kumwekea dawa ya kulevywa na kumfanyia tendo la ngono binti bila ridhaa yake.
Wakili wa gavana huyo, Imbambo Engulu ametupilia mbali tuhuma hizo na kushutumu mahakama ya jimbo hilo kwa kumzuia gavana huyo bila kujali cheo chake.
"Kushikwa kwake ni kama uonevu, tuliomba wamuzuie kwanza nyumbani kwake badala ya kumuweka gerezani moja kwa moja, majaji hawakukubali ombi letu, Nawambia kweli kuwa gavana hakufanya kitendo hicho, ni uongo."
Waziri wa sheria, Faida Mwangiliwa ambaye pia ni miongoni mwa wanaharakati wa haki za wanawake ameomba sheria kumhukumu vikali gavana huyo ikiwa tuhuma hizo zitathibitishwa na mahakama.
Kesi za ubakaji zimeripotiwa nyingi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, idadi kubwa ya kesi hizo zimefanywa na waasi na wanajeshi wa taifa hususan mashariki mwa DRC.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Kongo imeadhibu askari kadhaa na maofisa wa jeshi la Kongo wengi kwa kuwapa kifungo cha maisha. Anayekutwa na hatia kwa kosa la ubakaji nchini humo ni kifungo cha maisha gerezani.
BBC

No comments:

Post a Comment