Sunday, 22 April 2018

Hali ya uzalishaji mazao ya chakula imeimarika nchini - Serikali


Kassim Majaliwa

Mary Meshack, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini imeimarika na kufikia tani milioni 15.9 kwa msimu wa mwaka 2016/2017 na 2017/2018 sawa na kuwa na ziada ya tani milioni 2.6.

Pia Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekeleza mkakati wa kuiwezesha Wizara ya Kilimo kuongeza uwezo wa hifadhi ya Taifa ya chakula kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Aprili 21, 2018) wakati akiweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula, Kizota  mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema mkakati huo utahusisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa nje ya nchi na hivyo kutoa fursa za ajira na kuwaongezea kipato wananchi.

Amesema Serikali imefungua mipaka na inaendelea na jitihada za kutafuta masoko ya nje pamoja na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa kujenga maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo mengine yenye uzalishaji mkubwa wa chakula.

Pia Waziri Mkuu amewasihi wananchi kutumia fursa za kiuchumi kwenye maeneo ambayo mradi huo utatekelezwa ili kuboresha na kuinua hali zao kiuchumi hivyo watakuwa na uwezo wa kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huo mkubwa ambao baada ya kukamilika utakuwa na faida kubwa kwa Taifa, hivyo amewataka viongozi wa NFRA wahakikishe kwamba hakuna mahindi yatayoharibika katika maghala yao.

”Mikakati ya Serikali ni kuhakikisha NFRA inakuwa na uwezo wa kuhifadhi akiba ya kutosha ya chakula kwa ajili ya dharula lakini pia kuweka mazingira rafiki ya kuwezesha wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi bila vikwazo”.

Hata hivyp, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango na wakuu wa mikoa ambayo mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wahakikishe wanatimiza wajibu wao ili mradi ukamilike kwa wakati.

Naye kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankuba amesema mradi huo unatekelezwa katika maeneo manane ya Kanda za Wakala huo ambayo ni Dodoma (Dodoma), Mpanda (Katavi), Songea (Ruvuma), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga (Shinyanga), Babati (Manyara).

Vumilia amesema katika Kanda ya Dodoma wanajenga vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na kufanya kanda hiyo kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 59,000 kutoka uwezo wa sasa wa tani 39,000.

Amesema Serikali ya Tanzania na ya Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.

“Utekelezaji wa mikataba kati ya NFRA na wakandarasi ulianza Desemba 2017 ambapo muda wa utekelezaji ni miezi 18 tangu tarehe rasmi ya kuanza utekelezaji wa mikataba ya wakandarasi, hivyo kabla ya 2020 utakuwa umekamilika”.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai , Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira  na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Wengine ni Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi na  Ajira, Anthon Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo Dk. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Balozi Krzysztof Buzalski.

No comments:

Post a Comment