Tuesday, 24 April 2018

Israel yamwagia sifa Magufuli


Waziri wa Sheria wa Israel, Ayelet Shaked (kushoto), akizungumza wakati wa kongamano hilo, katikati ni waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.


SERIKALI ya Israel imempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kurejesha uhusiano unaolenga kuziimarisha nchi hizo mbili kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Sheria wa Israel, Ayelet Shaked wakati wa Kongamano la Tano la Biashara na Uwekezaji kati ya Israel na Tanzania.

“Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwetu na tunataraji kuuzindua rasmi juma lijalo”, amesema Waziri Shaked.

Ameongeza kuwa kwa zaidi ya miongo minne Tanzania na Israel hazikuwa na uhusiano wa kiuchumi wala ya kisiasa na kuongeza kuwa sasa nchi yao iko tayari kuwekeza nchini.

Waziri huyo ameeleza kuwa ni mara yake ya kwanza kufika Afrika na yuko tayari kuja na familia yake kwa ajili ya kufanya utalii Zanzibar na kwenye mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewakaribisha waisraeli kuwekeza nchini kwani Tanzania ni kitovu cha uwekezaji kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kutokana na amani iliyopo. Pia ameitaja nchi hii kuwa ni lango la biashara kwa nchi za kiafrika zinazoizunguka.

“Israel mnakaribishwa kuwekeza hapa Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji ni mazuri, tunayo ardhi nzuri kwa kilimo, tunayo maziwa, mito kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, hivyo hakuna mtakachokikosa endapo mnataka kuwekeza kwenye kilimo”, amesema Mwijage.

Waziri Mwijage ameongeza kuwa Tanzania iko tayari kuwekeza katika kilimo, viwanda vya dawa, Tehama, utalii, uzalishaji wa sukari na uongezaji thamani kwenye madini, na hivyo kuwahakikishia kuwa Serikali inaunga mkono suala la uwekezaji.

Naye balozi wa Israeli kwa nchi za Tanzania , Kenya, Uganda, Malawi na Shelisheli, Noah Gal Gendler amesema Serikali ya Rais Magufuli imeonesha mabadiliko makubwa ya ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kwa muda mfupi.

“Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 46 hakuna waziri hata mmoja kutoka Israeli amewahi kuitembelea Tanzania, lakini ndani ya wiki mbili wamefika mawaziri wawili kutoka nchini kwetu,” amesema Gendler.

Ameongeza kuwa katika kuimarisha sekta ya Afya, Israeli itajenga wodi za wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, na kituo cha huduma kwa watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Kongamno hilo ni la tano kufanyika hapa nchini likiwa na lengo la kuonesha fursa za uwekezaji zitakazotekelezwa baina ya wafanyabiashara wa Israeli na Tanzania.

Rais Dk. John Magufuli.

No comments:

Post a Comment