Wednesday, 18 April 2018

Jecha amaliza muda wake wa uongozi


Jecha Salim Jecha (wa kwanza kushoto)

Mwandishi Wetu, Zanzibar

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha amemaliza muda wake wa majukumu ya tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kilichoanzia Aprili 30,2 013 hadi Aprili 29, 2018 ambapo yeye na wajumbe wa tume hiyo wamekabidhi ripoti yao ya kazi.

Akitoa taarifa yake kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Jecha amesema tume inaamini kwamba, mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa majukumu yake hasa ya kiuchaguzi yalitokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali na wananchi kwa jumla.

"Ndani ya miaka mitano tume imeweza kuendesha jumla ya chaguzi ndogo nne, zikiwemo chaguzi ndogo tatu za udiwani na chaguzi moja ya uwakilishi pamoja na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,2015 na ule wa marudio yake Machi 20, 2016.

“Tume imefanya mapitio ya majimbo ya uchaguzi na kubadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi, majina ya majimbo na kuongeza idadi ya majimbo kutoka 50 hadi 54", amesema Jecha.

Pamoja na hayo, Jecha ameendelea kusema "Tume imeweza kufanya uandikishaji wa wapiga kura kwa awamu mbili na kuliendeleza daftari la kudumu la wapiga kura sanjari na kuendesha programu mbalimbali za elimu ya wapiga kura kupitia vyombo vya habari, mikutano ya wadau, uchapishaji wa vipeperushi, majarida na makala mbalimbali".

Aidha, Mwenyekiti huyo amemueleza Dk. Shein kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imechaguliwa kuwa kiongozi wa Uchaguzi Mkuu wa nchini Congo utakaofanyika Desemba mwaka huu.

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar Dk. Shein ameipongeza tume hiyo kwa kutekeleza vema majukumu yake ndani ya miaka mitano kwa kuendesha chaguzi zote.

"Tume hii inastahiki pongezi kwa kufanikisha vema kazi waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuendesha chaguzi zote ukiwemo Uchaguzi Mkuu, chaguzi ndogo na ule uchaguzi wa marudio ambazo zote hizo zilifanywa kwa ufanisi mkubwa," amesema Dk. Shein.

Wajumbe wa tume hiyo ambao wamemaliza muda wao licha ya Mwenyekiti Jecha, wengine ni Jaji Abdul-hakim Ameir Issa, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Nassor Khamis Mohammed, Ayoub Bakari Hamad, Haji Ramadhan Haji na Salmin Senga Salmin ambao wote hao waliapishwa rasmi  Mei,4, 2013.

No comments:

Post a Comment