Tuesday, 17 April 2018

Jeshi la Polisi lawatia mbaroni washukiwa 368

Mkuu wa operesheni maalum za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Liberatus Sabas anayeonesha baadhi ya silaha walizokamata kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Wengine ni maofisa mbalimbali waliopo katika operesheni hiyo. (PICHA NA JESHI LA POLISI) 

Mwandishi Wetu, Mtwara

JESHI la Polisi nchini limewatia mbaroni washukiwa 368 na kukamata silaha mbalimbali katika oparesheni maalum inayoendelea kwenye ukanda wa Kusini unaojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Mkuu wa operesheni maalum za Polisi, Naibu Kamishna Liberatus Sabas akizungumza huku akionesha baadhi ya silaha zilizokamatwa katika operesheni hiyo, amesema kati ya watuhumiwa 368, 13 tayari wamefikishwa mahakamani, 152 wamekabidhiwa Idara ya Uhamiaji kwa hatua zaidi, tisa wapo chini ya upelelezi na 194 wapo chini ya uangalizi wa Polisi.

Sabas amezitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni pamoja na SMG mbili, Pistol tano, Shotgun moja na risasi 145, Visu 96, makoti ya sare za Jeshi la Msumbiji mawili, raba za Jeshi la Msumbiji jozi mbili pamoja na vifaa vya kutengenezea milipuko.

“Baadhi ya watuhumiwa ni wale waliokimbia katika operesheni yetu ya mkoa wa Kipolisi Rufiji baada ya kuwazidi nguvu na sasa nawaambia tu wajisalimishe kwani hatuna mchezo hata wakimbilie wapi maana tumepata taarifa kuwa wamejificha nchini Msumbiji lakini kule napo wameanzisha operesheni kama hii“. amesema Sabas.

Aidha, Kamanda Sabas amesema operesheni hiyo ni endelevu na inashirikisha vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama hivyo ametoa mwito kwa raia wema kuendelea kutoa taarifa za siri ili kuendeleza amani na usalama hapa nchini.

Hivi karibuni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Msumbiji alikutana na IGP Simon Sirro jijini Dar es Salaam ambapo walijadiliana namna ya kuboresha ushirikiano ili kupambana na uhalifu unaovuka mipaka.

No comments:

Post a Comment