Tuesday, 17 April 2018

Jiji Arusha kuongeza mashine za kukusanya ushuru
Wankyo Gati, Arusha 

HALMASHAURI ya jiji la Arusha inatarajia kuleta zaidi ya mashine 100 zenye thamani ya sh. 88,500,000 kwa ajili ya kukusanyia tozo za ushuru katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha. 

Hayo yamebainishwa jana na mweka hazina wake, Mbwana Msangi wakati akitoa ufafanuzi kuhusu uhaba wa mashine za kutolea risiti katika maeneo ya maegesho ya magari jijini Arusha.

Amesema uwepo wa mashine hizo utasaidia kuondoa changamoto iliyokuwepo katika ukusanyaji wa mapato hayo na kuongeza mapato zaidi ya halmashauri.

Amefafanua kuwa, hali ya ukusanyaji mapato kwa kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Machi mwaka huu imefikia bilioni 10.4 sawa na asilimia 79.

Ameongeza kuwa uwezo wa ukusanyaji mapato kwa mwezi ni sh. bilioni  1.1 ambapo hadi kufikia Juni mwaka huu watakuwa wamefikia lengo walilojiwekea la mwaka 20017/2018 wakusanye sh. bilioni 13.2.

Amesema uwepo wa mashine hizo utaongeza mapato zaidi kutoka vyanzo mbalimbali kwani hapo awali kabla ya kuwepo mashine za kutosha walikuwa hawakusanyi ipasavyo. 

 Amefafanua maeneo ambayo ndiyo vyanzo vya mapato hayo kuwa ni pamoja na maegesho ya magari, masoko, vyoo, vibanda vya stendi  na ushuru wa moramu ambapo katika fedha hizo asilimia tano inatengwa kwa ajili ya kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa vijana na wanawake.  

"Sisi kama halmashauri tumepitisha bajeti ya sh. 16.5 bilioni kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 na tunaamini tutakuwa na ukusanyaji mzuri ambao utaongeza kiasi kikubwa cha fedha na tutafikia lengo,” amesema Msangi. 

Msangi amesema serikali imeshatoa mwongozo na kusitisha mkataba na kampuni ya Max malipo ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, hivyo serikali kuendelea kukusanya mapato ya vyanzo kupitia utaratibu waliojiwekea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ukusanyaji ushuru wa maegesho ya magari ya Kipipa Millers Company Ltd, Athuman Simba amesema uwepo wa mashine hizo utasaidia kuondoa changamoto ya uhaba wa mashine hizo na hivyo kuboresha zaidi ukusanyaji wa mapato ndani ya jiji la Arusha. 

No comments:

Post a Comment