Sunday, 8 April 2018

Kaimu mkurugenzi akagua maendeleo ya ujenzi majengo ya Nida
KAIMU mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa (Nida), Andrew Massawe ametembelea na kukagua hatua za ujenzi wa majengo ya ofisi katika mkoa wa Arusha na kukutana na viongozi mbalimbali wa mkoa huo kujadili maendeleo ya mchakato wa usajili wananchi linaloendelea nchini kote.

Ujenzi wa ofisi za Nida unaoendelea katika wilaya za Arusha, Arumeru na Longido ni mradi wa mkopo wenye masharti nafuu unaofadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini.


Anderew Massawe

Akizungumza na katibu tawala wilaya ya Longido mara baada ya kukamilisha ukaguzi wa majengo hayo, Massawe amesema yatawezesha Nida kufanikisha malengo ya usajili kwa asilimia kubwa.

Pia kurahisisha usafirishaji wa data kwenda makao makuu ya uzalishaji Vitambulisho kwakuwa majengo hayo yamejengwa kisasa na yana miundombinu ya kuwezesha uzalishaji wenye kukidhi vigezo vinavyohitajika kutokana na teknolojia inayotumika.

Akiwa katika wilaya ya Longido, mkurugenzi huyo alipokelewa na katibu tawala Toba Nguvila kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo ambaye ameishukuru Nida kwa hatua kubwa ya ujenzi wa jengo la kisasa kwenye wilaya hiyo mpya ya Longido ambalo si tu litasaidia kuondoa uhaba wa ofisi lakini pia kuwezesha taasisi nyingine kama Rita na uhamiaji kupata ofisi zitakazowahudumia wananchi kwa ufanisi mkubwa zaidi tofauti na hali ya sasa.

Kwa mujibu wa mkandarasi kampuni ya KT Korea, ujenzi wa majengo hayo unatazamiwa kumalizika mapema mwezi Mei mwaka huu na kukabidhiwa kwa Nida ili kuanza matumizi.

No comments:

Post a Comment