Thursday, 12 April 2018

Kasoro ya wito wa Makonda hakuna faradha – Waziri UmmyUmmy Mwalimu.

Peter Simon

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kasoro ya utaratibu ulioanzishwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni kutokuwa na faragha wakati wa kulizwa madai ya wazazi waliojitokeza kudai matunzo ya watoto wao.

Akizungumza jana Jumatano Aprili 11, 2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Ummy amesema kinachofanywa na Makonda kipo ndani ya sheria, hata watendaji wanaowasikiliza wanawake wametoka katika idara yake.

Amesema Wizara ya Afya inaunga mkono jitihada hizo, kwamba kasoro zilizojitokeza ni kwa baadhi ya wanawake waliotelekezwa kwenda na watoto na kutojali haki za kuwalinda katika hatua hizo za awali za mashtaka.

“Makonda amefanya kitu kizuri mwamko umekuwa mkubwa, ni sawa madawati yapo na ustawi wa jamii pia wapo lakini wengi wamekuwa wazito ila kwa sasa wameitikia wito kwakuwa yeye amewahimiza wanawake wenye matatizo hayo wafike kwake, kazi imekuwa nyepesi kwani hata wanaohudumia pale ni watu wetu wa Ustawi wa Jamii,” amesema Ummy.

Amesema kilichofanyika ni kama kuita kambi ambayo baadaye matokeo yatakayopatikana yatawanufaisha wanawake na ikiwa kutakuwa na ugumu kesi itakwenda mahakamani.

Hata hivyo, Ummy ametoa mwito kwa wanawake wanaokwenda kutoa mashtaka yao kuhakikisha wanalinda haki za watoto wao kwa kutowaonesha hadharani.

“Ninasema hili ni kosa la mwanamke mwenyewe, kwa mfano yule mtoto Mchina nimesikitika sana kule ni kumnyanyapaa amesambazwa mitandaoni kila mahali anazungumziwa, niwaombe Watanzania tujitahidi kuwalinda watoto hawa, tusisambaze picha zao kwa maslahi mazuri ya mtoto,” amesema Ummy. 

No comments:

Post a Comment