Friday, 13 April 2018

Kesi ya Sethi wa IPTL mahakama yatoa onyo upande wa mashtaka
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetoa onyo kwa upande wa mashtaka baada ya kushindwa kutekeleza amri yake ya kumpeleka mshtakiwa mmiliki wa IPTL, Harbinder Sethi kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi, amevitaka vyombo husika kuheshimu amri zinazotolewa na mahakama na kuzitekeleza.

Hakimu Shaidi amesema haipendezi mahakama kila wakati kutoa amri ambazo hazitekelezwi, na kuamuru tena mshtakiwa Sethi kupelekwa hospitali kabla hajatoa amri nyingine kwa mujibu wa sheria.

Awali, Wakili wa serikali, Nassoro Katuga amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia wameshindwa kumpeleka Sethi hospital kwa sababu maalumu ikiwemo kuhamishwa gereza kutoka Segerea kwenda Ukonga, pamoja na mshtakiwa huyo kuomba daktari wake kutoka Afrika Kusini awepo wakati akipatiwa matibabu.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na Wakili wa utetezi, Hajra Mungula akidai hazina msingi kwa sababu Sethi hakuwahi kuzungumzia suala la daktari. Pia Mungula amedai kuwa katika gereza la Ukonga Sethi haruhusiwi kuonana na mtu yoyote hata mke wake wa ndoa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment