Wednesday, 4 April 2018

Kituo chashaauriwa kuanzisha miradi


Chief Daudi Mrindoko

Suleiman Kasei

MWENYEKITI wa Asasi ya Wazalendo na Maendeleo Tanzania (Awamata), Chief Daudi Mrindoko ameushauri uongozi wa kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Bondeni Day Care and Oprhanace Center kilichopo manispaa ya Moshi, mkoa wa Kilimanjaro, kuanzisha mradi wa maendeleo kwa ajili ya kuwalelea watoto hao.

Mrindoko ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kilimanjaro ametoa kauli hiyo jana, wakati alipoalikwa kuungana na watoto hao kula chakula cha mchana ikiwa ni kusherekea sikukuu ya kufufuka kwa Yesu Kristu.

Amesema uongozi wa kituo hicho unapaswa  kujisajili jina la kibiashara brela na badae kujisajili Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), na manispaa ambapo itawasaidia kuomba tenda mbalimbali zitakazowaingizia kipato.

"Zipo tenda mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na manispaa ambapo mnaweza kuziomba na kupewa nyie kwa mfano kukusanya ushuru kwenye masoko yaliyo katika kata hii ya Bondeni na kujipatia kipato" amesema Mrindoko.

Mwenyekiti huyo aliupongeza uongozi wa kituo hicho kwa kutoa elimu na maadili mema kwa watoto hao na kupelekea kujiona wapo sawa na watoto wengine.

Mwenyekiti huyo aliiomba jamii yakiwamo mashirika binafsi kuona umuhimu wa kutembelea vituo mbalimbali vya watoto yatima na kuwafariji ili wasijione kama wametengwa na jamii.

Watoto hao yatima wapatao 202 katika kituo hicho walimwomba mwenyekiti huyo kuwafadhili kuwapeleka mbuga za wanyama ili waweze kujua mali asili ya nchi ambapo aliwaahidi kushirikiana nao kutafuta wadhamini ili waweze kutimiza adhima yao.

No comments:

Post a Comment