Tuesday, 24 April 2018

Kuna nafasi ya kura ya maoni kubadili mfumo wa uongozi nchini Kenya?


Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga (kulia) na rais Uhuru Kenyatta.

KUMEKUWA na mgawanyiko wa hisia katika majukwaa mbali nchini kama vile kwenye mitandao ya kijamii na hata wachangiaji mada hiyo kwenye vyombo vya habari nchini Kenya kuhusu kuidhinishwa mageuzi ya katiba kutoa nafasi zaidi za uongozi nchini.
Wafuasi wa upinzani wakionekana kushinikiza mwito wa kufanyika kura ya maoni nchini mahsusi kuikarabati katiba ili kuweza kutoa nafasi ya Uwaziri mkuu na manaibu wake, nafasi zitakazopewa vinara wa upinzani nchini.
Upande wa pili baadhi ya wafuasi wa serikali wanaonekana kupinga mwito huo wa kufanyika kura ya maoni na badala yake usubiriwe uchaguzi mkuu nchini mwaka 2022.
Miongoni mwa sauti nzito zinazosikika kushinikiza mageuzi hayo ya sheria ni za muungano wa upinzani nchini Nasa.
Baadhi ya wanasiasa katika chama hicho wamesikika hadharani wakitaka kura ya maoni iandaliwe nchini kuwajumuisha viongozi wao wakuu serikalini.
Mwito wa kutaka kura ya maoni umeongezeka hususan baada ya kilichokuja kutajwa kwa umaarufu nchini ‘the handshake’ kusalimiana kwa mkono kwa kinara wa upinzani Raila Odinga na rais Uhuru Kenyatta.
Wawili hao walikutana mwezi uliopita mbele ya umma kuashiria kuafikiana kisiasa kati ya wapinzani hao.
Ni hatua iliyonuiwa kuleta amani na utulivu nchini baada ya uchaguzi wa mara mbili mwaka jana nchini uliokumbwa na mzozo na mfarakano.
Katika uchaguzi wa August 2017 ushindi haukuja kama ilivyotarajiwa, na upinzani ulisusia uchaguzi uliofuata wa marudio Oktoba kutokana na walichokitaja kuwa hakuna nafasi ya kufanyika uchaguzi wa kuaminika nchini bila ya mageuzi walioyaitisha katika mfumo mzima wa uchaguzi.
Hata baada ya Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa marudio uhasama wa kisiasa uliendelea kuwepo Kenya hadi kukutana huko mwezi jana kwa Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kujaribu kuganga yajayo.
Kwa kauli yake mojawapo ya vinara wa upinzani - Gavana wa jimbo la Mombasa -Hassan Joho hivi maajuzi ameeleza kwamba ajenda kubwa iliyonayo upinzani nchini ni kutaka kujumuishwa ndani ya serikali, na kupambana na kutengwa kwa baadhi ya jamii nchini.
Joho ameongeza kwamba katiba ni ya wananchi, na ikifika wakati Wakenya wakitaka katiba ibadilishwe, itabadilishwa tu.

Msimamo wa serikali kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 27 mwaka jana ni kwamba haikuwa tayari kujadiliana kuhusu 'nusu mkate' - neno linalotumika kwa umaarufu kisiasa nchini kuashiria serikali ya muungano itakayohusisha ushirikiano na upinzani.
"Hatutokaa katika vyumba vya mikutano kujadiliana na kugawana uongozi serikalini. Ni wakenya wali na haki kuamua ni nani atakayekuwa rais," alisema Uhuru Kenyatta. Mara ya mwisho Kenya iliandaa kura ya maoni Agosti 4, 2010.
Wapiga kura waliulizwa iwapo wanakubali pendekezo la katiba mpya, iliyopitishwa na bunge Aprili Mosi, 2010.
Katiba hiyo mpya ilionekana kama hatua kubwa katika kuepuka ghasia zilizoshuhudiwa nchini baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
BBC

No comments:

Post a Comment